Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Hussein Mussa akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu taarifa ya kazi zilizotekelezwa na TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2021/2022 (Julai – Septemba 2021). Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Hussein Mussa akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu taarifa ya kazi zilizotekelezwa na TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2021/2022 (Julai – Septemba 2021).
Waandishi wa Habari wakichukua matukio wakati Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Hussein Mussa akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu taarifa ya kazi zilizotekelezwa na TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2021/2022 (Julai – Septemba 2021).
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga inaendelea kutekeleza Mkakati wake mkubwa wa kufuatilia fedha zilizotumika na zinazotarajiwa kutumika katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kukagua miradi yote inayotekelezwa ili kuhakikisha kuwa miradi hiyo inakuwa na thamani halisi ya fedha zilizotolewa.
Hayo yamesemwa leo Jumanne Novemba 2,2021 na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Hussein Mussa wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu taarifa ya kazi zilizotekelezwa na TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2021/2022 (Julai – Septemba 2021).
Mussa amesema katika mikakati ya utendaji kazi wa TAKUKURU mkoa wa Shinyanga kwa kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba 2021 wamejipanga kikamilifu kuendelea kufanya ufuatiliaji wa fedha za miradi na ukaguzi wa miradi ili kuhakikisha miradi inaendana na thamani halisi ya fedha zinazotolewa na Serikali na wadau wa maendeleo.
“Katika kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba 2021 tulijikita katika kuzuia rushwa kwenye miradi ya maendeleo inayotekelezwa mkoa mzima wa Shinyanga na miradi iliyopewa fedha za serikali na ufadhili wa wadau wa maendeleo kwa miradi inayotekelezwa katika mwaka wa fedha 2020/2021”,ameeleza.
“Katika ufuatiliaji huo kwa kipindi cha Julai – Septemba 2021 jumla ya miradi 10 yenye thamani ya shilingi 3,795,962,441/= ilitembelewa,ilikaguliwa na kutolewa ushauriwa namna bora ya kuiboresha ili miradi hiyo inakuwa na thamani halisi ya fedha iliyotolewa ili kuhakikisha hakuna ubadhirifu wala ufujaji wa fedha hizo”,ameongeza Mussa.
Amefafanua kuwa katika kipindi hicho cha Julai - Septemba 2021,TAKUKURU Shinyanga imefanya uchambuzi wa kubaini iwapo kuna mianya ya rushwa katika mapato ya stendi ya mabasi Maganzo,ukusanyaji wa ada za maegesho ya vyombo vya usafiri katika Manispaa ya Shinyanga na faini kwa wanaokiuka utaratibu wa maegesho pamoja na uchambuzi wa mfumo wa usimamizi wa mitihani katika vyuo vya kati ambapo Chuo cha Ufundi VET Shinyanga na Kahama vilifanyiwa kazi.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa TAKUKURU amesema wamepokea malalamiko 46 ambapo taarifa zinazohusu rushwa zilikuwa 27, kati ya hizo 20 uchunguzi wake unaendelea na malalamiko 7 uchunguzi wake umefungwa kwa kukosa ushahidi.
“Kwa mujibu wa taarifa tulizopokea kati ya Julai - Septemba Idara zilizolalamikiwa ni serikali za mitaa (15),elimu (6), ardhi (4), madini (4), ujenzi (3),afya (2), siasa (2), fedha (2), biashara (2),mahakama (2), kazi (2),maliasili (1) na barabara (1). Kesi zinazoendelea mahakamani ni 21. Kati ya hizo kesi mpya ni 3, kesi 4 ziliamuliwa mahakamani, kesi 2 zilishinda kwa watuhumiwa kutiwa hatiani na kulipa faini”,ameeleza Mussa.
Hata hivyo amesema TAKUKURU Shinyanga imeweka utaratibu wa kusikiliza kero za wananchi siku moja kila mwezi ‘TAKUKURU Inayotembea’ kwa kuwafuata wananchi katika maeneo yao ambapo wananchi wanapatiwa elimu ya kutosha juu ya madhara ya rushwa na namna ya kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kwenye ofisi za TAKUKURU.