SERIKALI YASITISHA UHAMISHO KWA WATUMISHI 'KIPAUMBELE KWA WALIO TAYARI KUFANYA KAZI VIJIJINI'

Na Dotto Kwilasa-Malunde 1 blog Dodoma.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Ummy Mwalimu amesema kwa sasa amesitisha masuala ya uhamisho kwa Watumishi wa umma wanaotaka kuhamia kwenye Majiji na kukataa kuishi vijijini na badala yake ataendelea kutoa nafasi za kubadilishana vituo vya kazi pale inapobidi.

Hayo yamejiri hivi karibuni Jijini Dodoma wakati wa mahafali ya 13 ya Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo (LGTI) huku Waziri huyo akisisitiza kuwa hali hiyo itatoa nafasi kwa wananchi wa pembezoni kupata huduma wanazostahili ikiwemo elimu na afya .

Amesema,sehemu za vijijini kuna uhaba mkubwa wa watumishi wa kada mbalimbali kutokana na watumishi wengi kukimbilia kufanya kazi Mjini na kwamba ili kumaliza tatizo hilo lazima wahitimu wote wawe tayari kuajiriwa na kupelekwa sehemu yoyote yenye uhitaji.

"Nimesitisha na nitaendelea hivyo mpaka tutakapofanya msawazo wa watumishi lazima ningalie kwa nini Ukerewe kuna walimu 100 wakati Kinondoni kuna walimu 2,000 tutaangalia mahitaji na waliopo ili kufanya maamuzi sahihi wakati wa kuhamisha,"amesema.

Aidha ameeleza kuwa ili kuwapa hadhi wanayostahili watumishi,Serikali imedhamiria kuboresha mazingira ya Vijijini ikiwemo kuanzisha Shule zenye mchepuo wa Kiingereza ili Watumishi wanaohitaji watoto wao kusoma shule hizo wapate fursa hiyo hali itakayo saidia kuacha kutamani kuishi Mjini.

Ametilia mkazo kuwa ili kukidhi mahitaji ya ajira nchini,Serikali itatoa kipaumbele cha ajira kwa wahitimu walio tayari kufanya vijijini huku akiwataka wanachuo wa chuo hicho (LGTI)wanaomaliza muda wao kujiandaa kisaikolojia kuishi maeneo yoyote watakapo pangiwa ili kuisaidia jamii.

"Mnapopata ajira muwe tayari kwenda kufanya kazi kwenye halmashauri za pembezoni (vijijini) na sio mkishapata tu mnaanza kuomba uhamisho kurudi Mjini,lazima mjifunze maisha ni popote mnapaswa kuridhika"amesisitiza

Aidha amesema Mamlaka ya Serikali za Mitaa itaendelea kuajiri wataalam wanaohitimu LGTI kwa kuwa wamepikwa kutumika vyema kwenye Serikali za Mitaa.

'Lazima tuwe wakweli,kwa sasa Serikali itatoa kipaumbele cha ajira kwa wahitimu walio tayari kufanya kazi Halmashauri za Vijijini ambapo kuna mahitaji makubwa ya Watumishi wa kada mbalimbali na si vinginevyo,"amesema Waziri Ummy na kuongeza;

“Watu wa kijijini pia wanahitaji huduma zenu, hivyo watumishi wanahitajika kwenda kufanya kazi maeneo hayo na sio kunga’ang’ania kubakia mjini wakati wote, kila mtu anataka Dodoma Jiji, Kinondoni, Arusha Jiji, Mwanza Jiji nani akae Mpimbwe, Uvinza, Kilindi, Rufiji,” amehoji Waziri huyo.

Wakati huo huo amesema Serikali itaendelea kuboresha na kutatua changamoto zilizopo Chuoni hapo ili kuboresha huduma za kijamii na kuongeza umakini wa masomo kwa wanachuo hao.

Amesema katika bajeti ya 2022/2023 watatenga fedha kea ajili ya Ujenzi wa bweni moja lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 2,500 ili wanafunzi wakae kwenye mazingira ya Chuo ambayo ni salama.

Aidha alisema atapigania ujenzi wa barabara ya lami kutoka Ihumwa hadi Hombolo kurahisisha hali ya usafiri na kukuza uchumi .

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Chuo cha Serikali za Mitaa, Profesa Joseph Kuzilwa ameiomba Serikali kuwezesha ujenzi wa barabara ya Ihumwa - Hombolo kwa kiwango cha lami ili kuweza kufika kiurahisi chuoni hapo tofauti na sasa ambavyo miundombinu hairidhishi.

Naye Mkuu wa Chuo hicho Dk. Mpamile Madale amesema chuo hicho kinakua siku hadi siku na kuongeza udahili na wanafunzi waliohitimu mwaka 2021 ni 6,021.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post