Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UVCCM KUSIMAMIA MIKOPO YA ASILIMIA 10 KWA VIJANA ILETE TIJA

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) mkoa wa Shinyanga, Baraka Shemahonge akikagua mizinga ya nyuki iliyotekelezwa na kikundi cha vijana cha Jitegemee kilichopo katika eneo la Zongomela,(Picha na Salvatory Ntandu).

Na Salvatory Ntandu - Kahama
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) mkoa wa Shinyanga, Baraka Shemahonge amewataka vijana wanaopatiwa mikopo ya asilimia 10 na serikali kuwa waaminifu ili iweze kuleta matokeo chanya katika miradi wanayoitekeleza kwenye jamii.

Kauli hiyo ameitoa jana wilayani Kahama katika ziara yake ya siku tatu yenye lengo la kuangalia uhai wa chama, utekelezaji wa ilani ya chama hicho sambamba na kukagua miradi mbalimbali ya vikundi vya vijana waliopatiwa mikopo na halmashauri ya manispaa ya Kahama.

Alisema licha ya halmashauri kuendelea kuwapatia mikopo vijana wapo baadhi yao sio waaminifu pindi wanapopatiwa mikopo hushindwa kurejesha kwa wakati na kusababisha serikali kupata hasara kinyume na malengo ya fedha hizo na kuwataka vijana kuwa mfano bora katika ujeshaji wa fedha hizo.

“Nimekagua shughuli zinazotekelezwa na vikundi vya vijana vya Tujitegemee,na mshikamano ambavyo vimepatiwa mkopo wa shilingi milioni 70, nimeridhika na kazi wanazozitekeleza,vijana wengine waige mfano wa vikundi hivi ambavyo mpaka sasa vimeweza kurejesha mikopo yao kwa wakati,”alisema Shemahonge.

Afisa Maendeleo ya Jamii wa halmashauri ya manispaa ya Kahama, Franael Rubeni alisema kuwa katika bajeti ya mwaka huu wa fedha wametenga zaidi ya shilingi milioni 150 kwa ajili ya mikopo ya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu na kuwataka vijana kujitokeza kwa wingi kunufaika na fursa hiyo.

“Vikundi vya wanawake ndio wanaongoza katika urejeshaji wa mikopo ikilinganishwa na vijana,licha ya kuwapatia elimu ya mikopo lakini wengi wao wamekuwa wakishindwa kuendeleza miradi wanayoianzisha na kusababisha serikali kupata hasara licha ya kupatiwa mikopo hiyo,”alisema Rubeni.

Mwenyekiti wa kikundi cha vijana cha msikamano kilichopo katika eneo la viwanda vindogo Zongomela, Ally Ramadhani aliiomba halmashauri hiyo kuwaongezea mkopo baada ya kumaliza deni lao kwa wakati ili kuwawezesha kunufaika na fursa ya utengenezaji wa madawati kwa sasa.

“Tulipata mkopo wa shilingi milioni 40 tumerejesha kwa wakati kwa sasa tunaomba kupatiwa shilingi milioni 100,sambamba kandarasi za utengenezaji wa madawati zinazotolewa na halmashauri kupitia fedha za IMF za UVIKO 19 zilizotolewa na serikali ya awamu ya sita,”alisema Ramadhani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com