Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MWAMBE AELEZA MWELEKEO WA SEKTA YA UWEKEZAJI MIAKA 60 YA UHURU



Waziri wa nchi Ofisi ya waziri Mkuu -uwekezaji Geoffrey Mwambe akiongea na Waandishi wa habari kuhusu Mafanikio ya Wizara hiyo kufikia miaka 60 ya uhuru

Na Dotto Kwilasa_Malunde 1 blog,Dodoma

SERIKALI imesema , katika jitihada za kuhamasisha uwekezaji wa kimkakati, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesajiri jumla ya miradi mikubwa ya kimkakati 43 inayotarajia kuwekeza kiasi cha dola za Marekani Milioni 12,278.00  huku ikitarajiwa kutoa ajira  130,720 

Hayo yamesemwa leo Jijini hapa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Geoffrey Mwambe  Jijini Dodoma wakati  akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara na kusema kuwa  miradi hiyo inahusisha sekta mbalimbali, ambazo ni Kilimo, Uzalishaji Viwandani, Majengo ya Biashara/Ujenzi na Madini.

Aidha amesema kuwa baadhi ya miradi iliyofanikishwa kupata hadhi ya uwekezaji kupitia NISC ni pamoja na Mradi wa Mount Meru Millers, Mlimani City, Dangote Industries Limited, Mtibwa Sugar Estates Ltd, Kagera Sugar Estate, Kilombero Sugar Company, Kilombero Plantations Limited (KPL), Tanga Cement Company Limited, TANCOAL Energy Limited, Goodwil Ceramics (Tz) Limited”,alisema Mwambe.

Vilevile amesema kuwa mifumo ya kielektroniki imeboreshwa kwa upande wa Cheti cha Uwekezaji, Usajili wa Kampuni, Kibali cha Kazi na Ukaazi maombi yote yanachakatwa katika mfumo wa kielektroniki.

“ Pia, taasisi zote zilizopo katika Kitengo cha Huduma za Mahali pamoja zinapokea malipo ya huduma zao kwa mfumo wa GePG hivyo kurahisisha malipo”amesema.

Pamoja na hayo ametaja mafanikio ya uwekezaji kwa serikali ya  awamu ya sita kwa kipindi cha miezi sita kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa usajili wa miradi ya uwekezaji yenye thamani ya dola za Marekani bil.3.5 ambapo ni sawa na tril.8.050,ambapo itatoa ajira za moja kwa moja elfu 38.

“Taarifa ya ulinganifu kwa kuzingatia miradi iliyoandikishwa TIC peke yake katika kipindi cha miezi sita ni 164 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.158 sawa na Shilingi za Tanzania trilioni 7.267”,amesema.

“ Usajili wa miradi hii ni sawa na ongezeko la takriban asilimia 500 ikilinganishwa na usajili kwa kipindi kama hiki mwaka jana ambapo miradi iliyosajiliwa ilikuwa na thamani ya Dola za Marekani milioni 647.43”,amesema.

Ameeleza kuwa taarifa za ulinganifu kwa kipindi kama hicho mwaka jana zinapatikana kutoka TIC ambapo kwa kipindi cha awamu hii miradi ya TIC itatoa ajira 32,715 ikilinganishwa na ajira elfu 10 kwa kipindi kama hicho mwaka jana na kwamba ongezeko hili ni zaidi ya asilimia 300 na kielelezo cha hatua kubwa kwa serikali ya mafanikio kwa serikali ya awamu ya sita.

Aidha Waziri Mwambe alitaja mafanikio katika sekta ya uwekezaji ambapo alisema kuwa kutokana na jitihada za Serikali za kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji, uwekezaji wa ndani  na ule wa kutoka nje  umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka.

“Mafanikio hayo yanaweza kupimwa kwa vigezo vitatu vinavyotumika kupima kiwango cha uwekezaji kwa nchi ambavyo ni Uwiano wa Uwekezaji na Pato la Taifa pamoja na Kiwango cha Uwekezaji Kutoka Nje na kiwango cha Ukuzaji Rasilimali kwa kila mwaka”,alisema Mwambe.

Amesema kuwa tangu Serikali ilipoanza kutekeleza Sera ya Taifa ya Uwekezaji na Sheria ya Uwekezaji Tanzania, wastani wa uwekezaji unaopimwa kwa kuangalia uwiano wa uwekezaji yaani Ukuzaji Rasilimali kwa Pato la Taifa umekuwa ukiongezeka.

“Takwimu zinaonesha uwiano wa ukuzaji rasilimali kwa Pato la Taifa umekua kutoka asilimia 14.7 mwaka 1997 hadi asilimia 39.7 mwaka 2019. Hivi ni viwango vikubwa ukilinganisha na wastani wa nchi za Afrika wa asilimia 21 – 22 na nchi zilizoendelea wa asilimia 23 hadi 25”,alisema.

Akizungumzia upande wa uwekezaji kutoka nje ya nchi Waziri Mwambe amesema kuwa uwekezaji wa mitaji kutoka nje umekuwa ukiongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 0.73 mwaka 1996 hadi Dola za Marekani bilioni 2.18 mwaka 2013 na hadi Dola za Marekani bilioni 1.01 mwaka 2020.

Hii ni sehemu ya ratiba ya mikutano ya Mawaziri na vyombo vya habari kuhusu historia ya Tanzania tangu ilipopata Uhuru hadi sasa kwa kila Sekta ambayo imeanza   Novemba 2, mwaka huu na  kuratibiwa na Idara ya Habari – MAELEZO kwa kushirikiana na Sekta husika.

Aidha shughuli hizo za maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru zitahusisha Wizara na Taasisi zote za Serikali kuelezea hatua ambazo kila sekta imepiga tangu tulipopata Uhuru, tulipo sasa na tunapoelekea. 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com