Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAHUNI WAVAMIA KANISA,WAIBA KISHA KUCHAFUA OFISI YA MCHUNGAJI KWA KINYESI


Wakazi wa kaunti ya Vihiga nchini Kenya wameachwa na mshtuko baada ya watu wasiojulikana kuvamia Kanisa la Mumbita Church of God Luanda na kujisaidia ndani ya Ofisi ya mchungaji.

Tukio hilo limelazimisha Church of GOD Afrika Mashariki (Kenya) kuandaa sherehe ya utakaso inayotarajiwa kufanyika Jumanne, Novemba 9,2021 ili kufukuza pepo na kuweka wakfu tena wa kanisa la Mumbita.

 Kulingana na mkurugenzi wa ustawi wa jamii katika mkutano mkuu wa kanisa hilo Wycliffe Ochieng, wezi hao pia waliiba lita 40 za rangi zilizokuwa zimehifadhiwa ndani ya kanisa hilo.

 Ochieng ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Maendeleo katika kanisa la Mumbita Church of God, alisema kuwa washukiwa hao lazima walivamia kanisa hilo Jumapili usiku.

"Kanisa letu lina usalama wa kutosha ikilinganishwa na mengine, lakini tulifika asubuhi na kukuta milango wazi," alisema.

 “Tulipoingia ndani kufanya uchunguzi, tulishtuka baada ya kupata dalili kuwa watu flani walivamia eneo hilo. Bidhaa mbalimbali ziliibiwa na ofisi ya mchungaji mkuu kuchafuliwa. Pia kulikuwa na sigara mbili na tochi ndogo iliyokuwa imeachwa sakafuni,” aliongeza Ochieng. 

Duru zilionyesha kuwa kisa hicho katika Kanisa la Mumbita ni cha tano katika msururu visa vya uvamizi wa makanisha huko Vihiga.

 Katika visa hivi vingi, wezi wamekuwa wakiacha kinyesi ndani ya makanisa ambayo wanavamia.

 Mwaka huu tu, makanisa matatu katika kata ya Mwibona pekee, ikiwa ni pamoja na Wemilabi Church of God, yamevunjwa na wahalifu na mali kuibiwa.

 Kulikuwepo na kisa kingine mnamo Agosti ambapo wahalifu walivamia kanisa la ACK St Mark, parokia ya Emako, na kuiba mali ya thamani ya Ksh 150,000 na kama ilivyo ada wahalifu hao waliacha kinyesi.

Joash Owila, mkuu wa ACK St Mark, parokia ya Emako, aliwaonya wahalifu dhidi ya kuvunja makanisa huku akibainisha kuwa wanaalika ghadhabu ya Mungu juu ya maisha yao. Pia aliwataka washukiwa watubu.

Chanzo - Tuko News

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com