Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WIZARA YA ARDHI YAJIVUNIA MAFANIKIO 6 MIAKA 60 UHURU...IMO KUTATUA MIGOGORO YA ARDHI 149,081

 

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,William Lukuvi 

Na Dotto Kwilasa - Malunde 1 blog Dodoma.

SERIKALI kupitia Wizara  ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imesema  inasherehekea miaka 60 ya uhuru wa Tanzania bara huku  ikijivunia mafanikio sita  ikiwemo kutatua    jumla ya migogoro ya ardhi 149,081 kiutawala. 

Mambo mengine ni  kupanga,kupima ardhi,kuwezesha wananchi kuwa na makazi bora, kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi,kuboresha mifumo na kutengeneza fursa za uwekezaji.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,William Lukuvi wakati akizungumza na Waandishi wa Habari leo  Jijini hapa kuhusu mafanikio ya Wizara hiyo ndani ya miaka 60,ikiwa ni sehemu ya fursa ambayo imeandaliwa na Idara ya Habari-maelezo kwa Wizara zote Nchini kueleza mafanikio yake tangu uhuru.

Waziri Lukuvi alisema katika miaka 60 ya uhuru wa Tanzania bara Wizara yake ,imeweza kutatua migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini na kwamba baada ya uhuru, utatuzi wa migogoro ya ardhi ulikuwa unafanyika kupitia mabaraza ya kimila na mfumo wa mahakama za kawaida.

Hata hivyo alieleza kuwa utatuzi wa migogoro ya ardhi kupitia mfumo wa mahakama ulibainika kuwa na changamoto za mrundikano wa mashauri na matumizi ya mbinu nyingi za kisheria katika utatuzi wa migogoro na kutokana na changamoto hizo ilipelekea Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 ilielekeza uanzishwe mfumo mahsusi wa utatuzi wa migogoro ya ardhi.


“Hivyo, Sheria ya Mahakama za Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi Na. 2 ya mwaka 2002 (Sura ya 216) ilitungwa na kubainisha mfumo maalum wa utatuzi wa migogoro ya ardhi unaojumuisha Mabaraza ya Ardhi ya Vijiji, Mabaraza ya Kata, Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya, Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa,”alisema.


Pamoja na hao Waziri Lukuvi alisema tangu kutungwa kwa sheria hiyo mwaka 2002, jumla ya mashauri 214,588 yalifunguliwa na mashauri 187,618 yameamuliwa.


Aidha, Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya yameanzishwa katika Wilaya zote 139 ambapo kati ya hayo, Mabaraza 60 yanatoa huduma. Dhamira ya Wizara ni kuhakikisha kuwa Mabaraza katika Wilaya zote nchini yanatoa huduma. 


Aidha, Wizara imeendelea kushughulikia migogoro ya ardhi ambayo imekuwa kero kubwa nchini kadri inavyojitokeza kwa njia ya kiutawala.


Alisisitiza kuwa  Migogoro hiyo ipo katika sura mbili ambazo ni migogoro ya mipaka ya kiutawala na migogoro inayotokana na mwingiliano wa matumizi ya ardhi.


Aidha, kupitia tathmini iliyofanyika imebainika kwamba vyanzo vya migogoro ni pamoja na ongezeko la watu, na mwingiliano wa matumizi ya ardhi kutokana na mahitaji mbalimbali ya watumiaji.


Wizara imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali ya kushughulikia utatuzi wa migogoro ya ardhi nchini.


Lukuvi alitumia nafasi hiyo kuitaja Mikakati hiyo ni pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu utatuzi wa migogoro kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali za Mitaa na kuanzisha madawati ya malalamiko katika ofisi za ardhi za halmashauri nchini pamoja na programu ya ‘Funguka kwa Waziri.


Aliyataja mafanikio mengine ni : “Tumepanga; Tumepima; Tumemilikisha; tumewawezesha wananchi kuwa na makazi bora; Tumeboresha mifumo; Tumetengeneza fursa za uwekezaji; Tumeweka mfumo mzuri wa utatuzi wa migogoro na tumesogeza huduma za ardhi karibu kabisa na wananchi.  


Waziri Lukuvi amesema jumla ya maeneo 496 yametangazwa kuwa ya kupangwa nchini.


Amesema kutangazwa kwa maeneo hayo kumewezesha kupangwa, kuendelezwa na kusimamiwa kimji kwa kuzingatia Sheria ya Mipango miji Sura ya 355. iii)


Amesema katika maeneo yalioendelezwa kiholela na ambayo yalikuwa ni mtaji mfu kwa wananchi tumerasimisha makazi 1,992,245 na kuwezesha wananchi hawa kuwa rasmi, usalama wa milki zao, na hadhi ya kukopesheka.  


Amesema kuipanga ardhi kumewezesha upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya uwekezaji katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa azma ya Serikali ya kujenga uchumi shindani wa viwanda kwa maendeleo ya watu. 


“Katika kutimiza azma ya Serikali ya kuwa na ardhi ya uwekezaji, ardhi yenye ukubwa wa ekari 885,144 zilitengwa na kumilikishwa kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwa shughuli mbalimbali ikiwamo viwanda, kilimo, hoteli na biashara.


Pia ardhi yenye ukubwa wa ekari 224,439.4 zimetengwa kwa ajili ya uwekezaji kupitia Mipango Kabambe ya miji, mipango ya matumizi ya ardhi ya Wilaya na Vijiji,”amesema.


Vile vile,amesema wamesimika   mtandao wa alama za msingi za mfumo huo nchi nzima katika kila mkoa na kila wilaya kwa umbali wa kilomita 40.


“Hii imewezesha kila mahali kupimwa bila ya kuwa na shida za alama za kuanzia. Aidha, mfumo huu umepunguza gharama za upimaji na kuongeza kasi ya upimaji wa ardhi nchini,”amesema. 


Pia,wamenunua vifaa vya upimaji vya kisasa na kuvisambaza katika mikoa yote na baadhi ya halmashauri.


hizo kumewezesha wananchi kupata huduma za ardhi karibu na maeneo yao, kwa wakati na pia kupunguza gharama za kupata huduma hizo. Ili kuimarisha usimamizi wa sekta ya ardhi kwa ufanisi zaidi, mwaka 2018 Serikali iliwahamisha watumishi wa sekta ya ardhi waliokuwepo katika halmashauri mbalimbali kuwa chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Kiutendaji maafisa hao wanafanya kazi kwa karibu za mamlaka za upangaji ambazo ni Halmashauri. 


Aidha,Waziri Lukuvi amesema umilikishaji wa ardhi kwa wananchi umewapa fursa wananchi kuchangia pato la Taifa.


MIAKA 10 MAKUSANYO BILIONI  735.8


Waziri huyo amesema Wizara inakusanya maduhuli ya sekta ya ardhi kutoka katika vyanzo mbalimbali kama vile, kodi ya pango la ardhi,ada za upimaji wa ardhi na Machapisho Mbalimbali,ada ya uthamini,ada za usajili wa hati na Nyaraka Mbalimbali.


Amesema Mwaka 1996/97 wakati Wizara ya Ardhi ilipopewa  mamlaka ya kukusanya maduhuli yatokanayo na sekta ya ardhi walikusanya  shilingi bilioni 1.4.                


“Kwa miaka 10 ya hivi karibuni (Juni, 2011 hadi Jalai, 2021) tumekusanya jumla ya shilingi bilioni 735.8,”amesema 


“Maduhuli yatokanayo na sekta ya ardhi yameongezeka kutoka shilingi bilioni 1.4 kwa mwaka wa fedha 1996/97 hadi kufikia shilingi bilioni 121 katika mwaka wa fedha 2020/21

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com