Na Costantine Mathias, Bariadi.
MADIWANI wa Halmashauri wa Mji wa Bariadi mkoani Simiyu wameitaka Idara ya afya kusimamia utoaji wa huduma za afya pamoja na kushughulikia mfumo wa bima ya afya iliyoboreshwa (ICHF) ili wananchi waweze kupata huduma ipasavyo.
Wamesema licha wananchi kulipia fedha kwa ajili ya kupata huduma hiyo, lakini wamekuwa hawaonekani katika mfumo wa bima pindi wanapokwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya kupata matibabu.
Akizungumza kwenye kikao cha robo ya kwanza cha Baraza la Madiwani, kilichofanyika katika ukumbi wa Barideco mjini Bariadi Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo David Masanja amesema wananchi wanapokwenda kupata huduma za matibabu baadhi ya kadi za bima ya afya hazionekani kwenye mtandao.
Amesema madiwani na watendaji wa mitaa wamehamasisha kwa nguvu wananchi ili waweze kuchangia bima ya afya iliyoboreshwa kwa ajili ya kupata matibabu pamoja na familia zao, lakini wamekuwa hawapati huduma za matibabu.
‘’Changamoto kubwa kwenye bima ya afya iliyoboreshwa (ICHF) ni wananchi kutopata matibabu kutokana na kadi kutoonekana katika mtandao, tumeomba idara ya afya kupitia ofisi ya Mkurugenzi kusimamia upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wateja wa bima…suala hili la mwananchi kutopata matibabu kwa sababu bima yake haijasoma kwenye mtandao, lisionekane katika Halmashauri yetu’’ amesema na kuongeza.
‘’Magonjwa hayapigi hodi, yanakuja muda ambao hauna fedha, lakini ukiwa na bima iliyoboreshwa utapata matibabu…Halmashauri ya mji wa Bariadi imeweka wazi kwenda kupata matibabu hata kama mtandao haufanyi kazi bali una kitambulisho cha bima’’ amesisitiza Mwenyekiti huyo.
Awali Diwani wa Kata ya Nyangokolwa Nkenyenge Charles amesema baadhi ya wateja wa bima ya afya iliyoboresha hawapati matibabu kutokana na kadi zao kutokuonekana kwenye mfumo wa bima, ambapo aliiomba idara ya afya kushughulikia changamoto hiyo ili wananchi waweze kupatiwa matibabu.
Diwani wa kata ya Guduwi Yohana Mnyumba ameomba ufafanuzi ili kuweka uelewa wa pamoja kwa madiwani ikiwa mteja (mgonjwa) bima yake haionekani kwenye mtandao kwamba anaweza kutumia utaratibu upi kupata matibabu ilhali ni mteja wa bima.
Akitoa ufafanuzi wa changamoto hiyo, Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri Marco Igenge amesema hawajawahi kukutana na changamoto hiyo kwa wagonjwa wa bima ya afya iliyoboreshwa na kwamba ikitokea hivyo, mteja (mgonjwa) anapatiwa huduma kwanza halafu watashughulikia mfumo baada.
‘’Hatujawahi kupata changamoto ya namna hiyo kwa mgonjwa, huwa tuna uhakika kuwa amejisajili na ikitokea hivyo tunampa huduma na baadae tunamsajili au kushughulikia mfumo, hatuwaachi wagonjwa hata kama hajajiunga na bima tunamhudumia’’ amesema Igenge.
Igenge amesema bima ya afya iliyoboresha (ICHF) hulipiwa shilingi elfu 30 kwa mwaka na kwamba inanufaisha watu wapato sita kwenye familia moja, ambapo alitumia nafasi hiyo pia kuwata madiwani kuendelea kuhamasisha wananchi kujiunga na bima hiyo ili wanufaike na matibabu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoa wa Simiyu Adrian Jungu, akiongea kwenye kikao cha Baraza la madiwani.
Diwani wa Kata ya Nyangokolwa Nkenyenge akichangia hoja kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya mji wa Bariadi.
Social Plugin