Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BONDIA AFARIKI KWA KUPIGWA MAKONDE KWENYE PAMBANO



Maswali yanaulizwa kuhusu taratibu za usalama katika ndondi ya Zimbabwe kufuatia kifo cha Taurai Zimunya baada ya kupigwa katika pambano mjini Harare.

Zimunya, 24, wa uzito wa Super bantam, alifariki siku ya Jumatatu, baada ya kuzimia wakati wa pambano lisilo la ubingwa siku ya Jumamosi.

Ni mara ya kwanza kwa bondia kufariki nchini Zimbabwe kutokana na majeraha aliyoyapata ulingoni.

Lawrence Zimbudzana, katibu mkuu wa Bodi ya Kitaifa ya Kudhibiti Ndondi na Mieleka ya Zimbabwe (ZNBWCB), anasema kuwa mipango ya uchunguzi bado haijashughulikiwa.

"Kwa sasa tutaangazia mazishi, na kisha tuketi na kuangalia masuala," Zimbudzana aliambia BBC Sport Africa katika mazishi ya Zimunya Jumatano.

Taarifa iliyotolewa na ZNBWCB ilisema kuwa "taratibu zote muhimu za matibabu zilifuatwa na msaada wa dharura wa matibabu ulitolewa mahali hapo kabla ya kupelekwa hospitali".

Zimunya alipigwa makonde kadhaa kichwani kabla ya kubanduliwa nje katika raundi ya tatu ya pambano la raundi sita.

Aliyekuwa mkufunzi wake Tatenda Gada alihuzunika, akihisi nyota huyo alikuwa na uwezo mkubwa.

"Tumeopokonywa mojawapo ya matarajio yetu mazuri," Gada alisema. "Nilifanya kazi na Taurai kwa zaidi ya miaka minne - nilimtazama akistawi na alikuwa mmoja wa nyota wajao katika fani hii."

Baba yake Zimunya, Samson, alikuwa bondia mahiri asiye wa kulipwa na alitarajia mtoto wake angebeba jina la ukoo na kuwa bingwa.

Ndondi ilikuwa imerejea tu Zimbabwe baada ya vizuizi vya kupambana na janga la corona kulegezwa.

Chanzo- BBC Swahili

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com