Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndg. Daniel Chongolo amesisitiza Chama kuendelea kusimamia kila fedha iliyopangwa kwa ajili ya maendeleo inashuka kwa wananchi na kutekeleza miradi ya maendeleo kama ilivyokusudiwa.
Katibu Mkuu ameyasema hayo, tarehe 13 Novemba, 2021 katika mapokezi wilayani Biharamulo Mkoa wa Kagera ambapo Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa inayoongozwa na Katibu Mkuu ipo ziarani katika mikoa ya Kagera, Geita, Kigoma, Katavi na Tabora.
Akizungumza katika mapokezi hayo Katibu Mkuu amesema,
"Bajeti ya mkoa kwa mwaka 2021/22 ilikuwa bilioni 294, mpaka sasa zimeshashuka zaidi ya bilioni 60, lakini Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, ameshusha Shilingi bilioni 20 mkoa wa Kagera kwa ajili ya maendeleo kama vile miundombinu ya elimu na afya kwa lengo la kuwaondolea wananchi kero ya kuchanga michango kwa ajili ya ujenzi wa madarasa kama ilivyokuwa hapo awali, na hizi ni fedha za ziada nje ya bajeti ya mkoa."
Katibu Mkuu amesisitiza kuwa "Kazi yetu sasa kama Chama ni kuhakikisha fedha hizo hazipotei hata senti moja, 'kutoa jicho' na sisi tumekuja hapa timu nzima, lengo letu kupita kila eneo kuhakikisha kila senti iliyoshuka haipotei na inakwenda kutafsiri matokeo halisi ya maendeleo kwa wananchi."
Aidha, Katibu Mkuu ameeleza pia lengo la ziara hii ni kuhimizana, kuhamasishana na kukumbushana taratibu za Chama chetu, ikiwa ni maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa ndani ya Chama chetu unaotarajiwa kufanyika hapo mwakani.
Awali akimkaribisha Katibu Mkuu, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kagera Ndg. Constansia Buhiye ameishukuru Sekretarieti ya Halmshauri Kuu ya CCM Taifa kwa ziara hii, kwani itaendelea kuhamasisha maendeleo na uhai wa Chama mkoani humo.
Social Plugin