CHUO KIKUU CHA GLASGOW KUONGEZA FURSA ZA TAFITI TANZANIA


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo akizungumza na Wanachuo na Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Glasgow Scotland leo Novemba 11, 2021. Chuo hicho kimejikita zaidi katika kufanya tafiti za masuala ya Mazingira, afya ya binadamu na wanyama. Chuo hicho kinafanya kazi kwa karibu na Taasisi za Tanzania ikiwa ni pamoja na TANAPA, TAWIRI, TAWA na Ifakara Heathy InstituteWaziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 26 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaoendelea Glasgow pamoja na wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Glasgow Scotland leo Novemba 11, 2021. Ujumbe huo wa Tanzania ulitembelea Chuo hicho kwa lengo la kujifunza na kubadilshana uzoefu katika masuala ya mazingira.

****************************

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika hifadhi ya mazingira husasan katika suala la kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Jafo amezitaja jitihada hizo kuwa ni pamoja kuanza kutumika kwa gesi majumbani, kwenye uendeshaji wa mitambo viwandani na kwenye magari badala ya dizeli na petroli pia matumizi ya mabasi yaendayo kwa kasi katika jiji la Dar es salaam.

Akizungumza na Wahadhiri na Wanachuo wa Chuo Kikuu cha Glasgow Scotland leo tarehe 10 Novemba 2021, Waziri Jafo ametoa rai kwa Chuo hicho kuongeza kasi katika kufanya tafiti za masuala ya Mazingira.

Amesema suala la Mazingira ni mtambuka na linahusisha sekta mbalimbali hivyo jitihada za pamoja zinahitajika katika kupambana na uharibifu wa mazingira ili kuwa na mazingira safi, salama na endelevu kwa faida ya vizazi vya sasa na vizazi vijavyo.

"Tanzania tumepiga hatua kubwa katika suala la hifadhi ya Mazingira kwa kusimamia kimkakati Sheria, Taratibu na Kanuni zilizopo" Jafo alisisitiza.

Waziri Jafo pia ametoa wito kwa uongozi wa Chuo Kikuu cha Glasgow kuendelea kutoa nafasi za tafiti mbalimbali katika suala la mazingira kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kutoa nafasi za ufadhili wa masomo kwa wa Tanzania kupitia Chuo hicho.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitivo cha Bioanuai, Wanyama na Afya wa Chuo Kikuu cha Glasgow Profesa Dan Haydon amesema Chuo hicho kimetoa takriban paundi 11 Milioni kudhamini na kuendeleza tafiti za kisayansi katika mifumo ikolojia iliyo endelevu, kulinda bioanuai, masuala ya afya ya binadamu na wanyama na uhifadhi wa mazingira.

“Kazi hizi za utafiti ni za msingi na tunaona fahari kushirikiana kwa karibu na taasisi mbalimbali za Tanzania kama vile TANAPA, TAWIRI na TAWA, tunapenda tushirikiane zaidi katika miaka ijayo” alisisitiza Profesa Haydon.

Waziri Jafo aliongoza ujumbe Tanzania katika ziara hiyo ya siku moja na alimbatana na Dkt. Agnes Kijazi, Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Profesa Dos Santos Silayo Mtendaji Mkuu, Wakala wa Misitu Tanzania, Mkurugenzi wa Mazingira Dkt. Andrew Komba na Bi. Farhat Mbarouk, Mkurugenzi wa Mazingira – Zanzibar

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post