MAKAMU Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo, Zanzibar Juma Duni Haji amejiuzulu nafasi hiyo, ili kugombea nafasi ya uenyekiti wa chama hicho, iliyokuwa ikishikiliwa na Maalim Seif Sharif Hamad aliyefariki dunia Februari 17 mwaka huu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Duni maarufu kama ‘ Bob Duni’ aliwasilisha uamuzi wa kujiuzulu nafasi hiyo Oktoba 30 baada ya kumwandikia barua Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu kuhusu hatua hiyo. Uamuzi Duni umekuja baada ya ACT- Wazalendo kutangaza mchakato wa kumpata mwenyekiti mpya.
Hayo yamebainishwa na Naibu Katibu wa Habari, Uenezi, Mahusiano na Umma wa ACT-Wazalendo, Janet Rithe ameeleza hayo leo Jumatatu Novemba Mosi, 2021 wakati akizungumza na wanahabari kuhusu maazimio ya kikao cha halmashauri kuu kilichoketi jana Jumapili Dar es Salaam.
“Uchaguzi wa kumpata mwenyekiti wa chama na mjumbe mmoja wa halmashauri kuu ya chama utafanyika Januari 29 mwaka 2021.Pia Kamati Kuu ya ACT- Wazalendo imevunja ngome ya wanawake baada ya kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi,” amesema Rithe.
Rithe amesema awali ngome ya wanawake ilikuwa inaongozwa na Mkiwa Kimwanga ambaye aliyekuwa mwenyekiti pamoja na Janeth Fussi aliyekuwa katibu, lakini kwa sasa ACT- Wazalendo imeunda kikosi kazi cha wajumbe watano ili kutekeleza jukumu hilo.
“Pavu Abdallah atakuwa Mwenyekiti, Bonifasia Mapunda (katibu), wakati Halima Ibrahim, Annamerrystella Mallack na Sevilina Mwijage watakuwa wajumbe wa kikosi kazi hiki. Watafanya kazi hii hadi pale uchaguzi utakaoitishwa tena,” amesema Rithe.
Social Plugin