Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HESLB YAFUNGUA DIRISHA LA RUFAA KWA SIKU TANO KUANZIA NOVEMBA 6, 2021




Na Mwandishi Wetu, HESLB,Dar es salaam

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) leo (Jumamosi, Novemba 6, 2021) imefungua dirisha la rufaa ili kuwawezesha waombaji ambao hawajapangiwa mikopo au wanahitaji kuongezewa viwango vya mikopo kwa mwaka wa masomo 2021/2022 kuwasilisha maombi ya rufaa zao.

“Dirisha hili litakuwa wazi kwa siku tano, kuanzia leo, Novemba 6 hadi 10, 2021 na ni fursa kwa wanafunzi wote, wa mwaka wa kwanza na wanaoendelea, kuwasilisha maombi yao ya kuongezewa viwango vya mkopo au kupangiwa kwa wale ambao hawajapangiwa hadi sasa,” amesema Dkt. Veronica Nyahende, Mkurugenzi wa Uchambuzi na Upangaji Mikopo wa HESLB.

Kuhusu utaratibu wa kuwasilisha maombi ya rufaa, Dkt. Nyahende amesema maombi yote ya rufaa yanapaswa kuwasilishwa kwa njia ya mtandao kama yalivyowasilishwa maombi ya msingi.

“Kupitia dirisha hili, tunawasihi waombaji mikopo kusoma maelekezo kwa makini na kuyazingatia … ikiwemo kuweka nyaraka zinazothibitisha uhitaji wao ambazo awali hawakuwa wameziweka,” amesisitiza Dkt. Nyahende.

Wakati huohuo, Dkt. Nyahende amefafanua kuhusu wanafunzi wanaoendelea na masomo na ambao walikuwa wameomba mkopo kwa mwaka 2021/2022 na kusema kuwa maombi yao yamechambuliwa na wale wenye sifa tayari wameshapangiwa mkopo.

“Hawa tunawaita ‘first time continuing applicants’, na tumeshawapangia na kuweka taarifa zao katika SIPA na kwa kuwa ni wazoefu, wakiingia wataona … maafisa mikopo wa vyuo pia wana taarifa zao,” amesema Dkt. Nyahende.

Kuhusu malipo ya fedha kwa wanafunzi waliopangiwa mikopo, Dkt. Nyahende amesema HESLB imeshatuma vyuoni fedha za wanafunzi wote wa mwaka wa kwanza ambao wamepangiwa mikopo na kuwakumbusha wanafunzi hao kufika katika ofisi za mikopo vyuoni ili kukamilisha taratibu za kupokea fedha hizo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com