............. ............................
MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu November 20,2021 amefanya ziara kwa vijiji na Vitongoji vya kata ya Ikungi kwa lengo la kuwahimiza wananchi na viongozi kushirikiana katika kusimamia miradi iliyopelekwa kwenye maeneo yao ili iwe na tija ikiwemo kuonyesha thamani halisi ya fedha.
Akizungumza katika ziara hiyo,Mtaturu ameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mhe Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha kupitia Mpango wa maendeleo na mapambano dhidi ya uviko 19 ambapo wilaya ya Ikungi imepokea zaidi ya Shilingi Milioni 781.7 kwa ajili ya miradi ya Sekondari kwa madarasa 40 na zaidi ya Shilingi Milioni 693.2 kwa ajili ya madarasa 21 kwenye shule shikizi.
"Mh Rais,mama yetu anaguswa na shida za wananchi,Fedha za UVIKO amezielekeza kwenye miradi ya maendeleo,hapa kwetu ametuletea Shilingi Bilioni 1.48 zinajenga vyumba vya madarasa kwenye shule shikizi na ujenzi wa Shule mpya ya sekondari ya Matongo," alisema.
Amesema kupitia fedha hizo jumla ya madarasa 40 kwenye shule za Sekondari, nyumba za walimu, majengo ya utawala vitajengwa kwenye kata zote 13 za jimbo la Singida Mashariki katika kipindi cha November hadi Disemba 2021.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Ikungi Abely Nkuwi amemshukuru mbunge Mtaturu kwa kuwasemea changamoto walizonazo kwenye kata yao.
"Mbunge wetu Mtaturu July 17,2021 alifanya ziara kwenye kijiji cha Matongo kitongoji cha Mau akakuta wananchi wanajenga shule na aliwaunga mkono,nafikisha salamu za wananchi wanaishukuru sana serikali kwa kuwakumbuka na kuwaletea fedha za kuboresha miundombinu ya shule itakayowasaidia wanafunzi kupunguza msongamano na mwendo mrefu kufuata shule,"alisema.
Amesema katika ziara hiyo mbunge alitembelea shule shikizi ya Mbughantigha na kukuta wananchi wamejenga madarasa mawili yakiwa yamefikia usawa wa renta na kuamua kuwaunga mkono Ili kumalizia ujenzi huo.
Awali afisa elimu Sekondari Mwalimu Ngwano John Ngwano amemuhakikishia mbunge na wananchi kuwa ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri ya Ikungi imejipanga kuhakikisha vifaa vya ujenzi vinafika maeneo yote kwa wakati. "Katika hili niwaelekeze watendaji kusimamia fedha hizi za serikali kwa uaminifu ili zitoe matokeo chanya kama Rais wetu alivyoelekeza wakati wa uzinduzi wa mpango wa maendeleo wa Taifa na uviko 19 Jijini Dodoma,".