Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo akimsikiliza mwakililishi wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Dkt. Ruth Kattumuri katika moja ya mikutano inayoendelea Glasgow Scotland. Jumuiya hiyo imeonyesha nia ya kuisaidia Tanzania katika jitihada za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mwakililishi wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Dkt. Ruth Kattumuri akizungumza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo katika moja ya mikutano inayoendelea Glasgow Scotland. Jumuiya hiyo imeonyesha nia ya kuisaidia Tanzania katika jitihada za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo akiwa katika picha ya pamoja na Mwakililishi wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Dkt. Ruth Kattumuri na Balozi wa Tanzania nchini Uingereza Dkt. Asha Rose Migiro mara baada ya kukamilika kwa kikao kazi baina yao.
*************************
Na Lulu Mussa
Scotland
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo leo Novemba 8, 2021 amefanya mazungumzo na mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Dkt. Ruth Kattumuri katika Mkutano unaoendelea Glasgow Scotland.
Waziri Jafo amesema kuwa Tanzania inatekeleza kimkakati Malengo endelevu ya maendeleo na kupitia mkutano wa COP 26 unaoendelea utawezesha Tanzania kupata rasilimali fedha na utaalamu utakaowezesha utekelezaji wa miradi na shughuli mbalimbali za kupunguza na kuhimili athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Amesema kuwa Tanzania imewasilisha Mchango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (Nationally Determined Contributions-NDC) katika Sekretarieti ya Mkataba wa mabadiliko ya tabianchi ambao umegawanyika katika sehemu kuu mbili ambazo ni: masuala yanayohusu kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi (adaptation); na masuala yanayohusu upunguzaji wa gesijoto (mitigation).
Ameyataja masuala yanayohusu kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi na sekta za vipaumbele kuwa ni kilimo, mifugo, misitu na wanyama pori, nishati, mazingira ya bahari na ukanda wa Pwani na uvuvi (bahari, maziwa, mito na maeneo oevu), maji na usafi wa mazingira, utalii, makazi ya binadamu, afya, miundombinu, majanga na masuala mtambuka ikiwemo jinsia, tafiti, fedha na teknolojia.
Aidha katika kuhimili mabadiliko ya tabianchi masuala mtambuka yatahuishwa ikiwa ni pamoja na jinsia, kujenga uwezo, tafiti na maendeleo na ubadilishanaji wa teknolojia baina ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea ili kuhimili mabadiliko ya tabianchi. Katika upunguzaji wa gesijoto, sekta za vipaumbele zilizobainishwa katika upunguzaji wa gesijoto ni pamoja na nishati, misitu, usafirishaji na udhibiti wa taka.
Nae Mkurugenzi wa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Andrew Komba ametoa rai kwa Jumuiya ya Madola kuongeza rasilimali fedha kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa nishati jadidifu na kuongeza kasi katika matumizi ya nishati mbadala na kujenga uwezo wa kitaasisi katika Majiji sita ya Tanzania ili kuwa mfano katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mazingira Zanzibar Bi. Farhat Mbarouk amesema kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi kwa Zanzibar ni kubwa katika sekta za utalii, kilimo pamoja na Uvuvi na kutoa rai ya kwa Jumuiya ya Madola kuongeza rasilimali fedha katika kujenga uwezo wa kitaasisi katika ukusanyaji wa takwimu za athari za mabadiliko ya tabianchi na kusaidia Zanzibar kuandaa Mpango wa usimamizi wa maeneo ya ukanda wa Pwani katika sekta ya Uchumi wa Bluu.
Kwa upande wake Dkt. Ruth Kattumuri amesema jumuiya hiyo iko tayari kuunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha suala la hifadhi ya mazingira linaenda sambamba na utekelezaji wa maendeleo endelevu.
Social Plugin