Meneja wa Kampuni ya GOPA CONTRACTORS Godfrey John, amewaomba radhi Wakulima katika Skimu ya Endagaw kwa kuchelewa kuanza ujenzi wa Miundombinu ya Mifereji na Ukarabati wa Bwawa kwa zaidi ya miezi miwili.
Akizungumza katika kikao kilichowashirikisha, Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Bi Janeth Mayanja, watendaji wa Tume na Wakulima wa Skimu hiyo, Meneja wa kampuni ya GOPA CONTRACTORS Bw, Godfrey John amekiri kampuni yake kushindwa kuanza shughuli za ujenzi katika Skimu hiyo kwa mujibu wa mkataba wa makubaliano na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na kwamba zoezi la ujenzi litaanza hivi karibuni kwa ubora na viwango vilivyoainishwa kwenye mkataba baada ya kutatua changamoto zilizoikabili kampuni yake.
Mhandisi wa Tume ya Taifa Umwagiliaji Bw, Juma Hamsini, ametoa onyo kali kwa mkandarasi huyo na kuongeza kuwa endapo kampuni yake itarudia kutenda kosa kama hilo, Tume ya taifa ya Umwagiliaji itaiweka kampuni hiyo katika orodha ya makampuni yanayotiliwa shaka kiutendaji hali itakayosababisha kampuni hiyo kukosa fursa ya ujenzi wa Miradi ya Miundombinu ya Umwagiliaji inayoratibiwa na Tume.
Kwaupande wake Mkuu wa Wilaya ya Hanang Bi, Janeth Mayanja, amemtaka Mkandarasi huyo kujenga Miundombinu kwa viwango na ubora kwa mujibu wa mkataba na kwamba atafuatilia ujenzi wa Mradi huo kwa karibu hadi utakapo kamilika.
Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ilisaini makubaliano na kampuni ya Gopa Contractors ya jijini Dar es Saalam, kujenga Mfereji mpya wenye urefu wa Mita Elfu mbili na Mianne (2,400) sanjari na kuongeza urefu mfereji wa zamani kwa kujenga Mita Miasaba na Sabini (770) pamoja na kuondoa Tope ndani ya bwawa linalotumika kumwagilia Skimu ya Endagaw.
Mkataba wa ujenzi wa miundombinu hiyo baina ya Tume na Mkandarasi Gopa Contractors ni wa zaidi ya Shilingi Milioni Miatisa Themanini.( Milioni 980) na ulisainiwa tarehe 31.08. 2021.
Mkuu wa Wilaya ya Hanang Bi, Janeth Mayanja (Katikati waliosimama),Mkurugenzi wa Kampuni ya Gopa Contractors (wa tano kulia(aliyevaa miwani) pamoja na Watendaji wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji katika eneo la kuhifadhia mitambo ya Mkandarasi mara baada ya kulikagua na kujiridhisha
Bakari Khamis – Diwani wa Endagaw akiwaonyesha Wahandisi wa Tume changamoto zilizopo katika Bwawa la Endagaw linalotumika kumwagilia Skimu ya Endagaw.
Social Plugin