KOCHA MPYA WA SIMBA SC ATAMBULISHWA RASMI..AKABIDHIWA FAILI LA YANGA


Baada ya kocha mpya, Mhispania, Pablo Franco kutambulishwa Jumamosi usiku, aliyekuwa kaimu kocha mkuu wa timu hiyo, Mnyarwanda, Thiery Hitimana amefichua kuwa atakaa chini na kocha huyo na kumuelezea kila kitu ikiwemo ukubwa wa mchezo wao ujao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya watani wao, Yanga.

Franco amejiunga na Simba kama kocha mkuu wa mkataba wa miaka miwili akitokea Qadsia ya Kuwait kwa ajili ya kuchukua mikoba Didier Gomes aliyeachana na timu hiyo hivi karibuni.

Mhispania huyo mwenye rekodi ya kuifundisha Getafe inayoshiriki Ligi Kuu ya Hispania na kocha msaidizi wa Real Madrid akiwa chini ya Julen Lepetegui na baadaye Santiago Solari ana kibarua cha mechi mbili kubwa muhimu kwa Simba ikiwemo dhidi ya Yanga inayotarajia kupigwa Disemba 11, mwaka huu jijini Dar es salaam.

Mhispania huyo ataanzia kwenye mechi moja ya ligi kuu kabla ya kuwavaa Red Arrows kwenye mechi mbili za Kombe la Shirikisho hatua ya mtoano ambaye baadaye atacheza dhidi ya Geita Gold kisha ndiyo atakutana na Yanga.

Hitimana alisema kuwa anajua wana kazi kubwa ya kuhakikisha wanarejea kwenye ubora wao hivyo hatosita kumpa mafaili yote kocha mpya ukiwemo mchezo wa Yanga kwa kuwa wanataka kuipeleka mbali timu hiyo.

“Suala la kocha mpya kwangu siyo shida kwa sababu maisha ya mpira ndiyo yamekuwa hivyo siku zote, leo inaweza kuwa imekaa hivi lakini kesho unaweza kukuta mambo yapo tofauti lakini jambo la msingi ni kuangalia kwetu na kocha mpya nini ambacho tunaweza kukifanya katika mechi ambazo zipo mbele yetu.

“Najua ni kwamba nitamwambia au kumpa ripoti ya mechi ambazo tumeshacheza na zile ambazo hatujacheza ili kuweka mikakati ya kupata matokeo, tuna mechi za mbili za Kombe la Shirikisho ambayo inahitaji mikakati na ile ya Yanga ili kuweza kujua tunapitia wapi, kucheza na Yanga na Simba ni presha kubwa hivyo mwalimu lazima apate nafasi ya kuwajua kwa kuwaangalia na kumwambia,” alisema Hitimana.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post