Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi imetupilia mbali hoja tatu zilizotolewa na upande wa utetezi katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi na kukipokea kitabu cha kumbukumbu ya mahabusu kama kielelezo.
Mbowe na wenzake hao, Halfan Bwire Hassan, Adamu Hassan Kasekwa na Mohamed Abdillahi Ling’wenya wanakabiliwa na kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Joachim Tiganga.
Uamuzi huo unahusu pingamizi la mawakili wa utetezi katika kesi hiyo, ambao walipinga kupokewa kwa kitabu cha kumbukumbu za mahabusu (Detantion Register – DR), cha Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam, cha mwaka 2020, kiwe kielelezo cha ushahidi upande wa mashtaka.
Mahakama hiyo imepokea kitabu hicho jana Jumatatu, tarehe 22 Novemba 2021, mbele ya Jaji Joachim Tiganga, akitoa maamuzi madogo ya mapingamizi ya mawakili wa utetezi
Upande wa mashtaka unaongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando uliiomba mahakama hiyo ikipokee kitabu hicho kuwa kielelezo cha ushahidi wake, kupitia kwa shahidi wa pili katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi, Ditektivu Koplo Ricardo Msemwa.
Hata hivyo jopo la mawakili wa utetezi linaloongozwa na Peter Kibatala lilipinga kitabu hicho kupokewa, huku wakitoa hoja tatu za pingamizi lao
Walidai kwamba hakuna amri ya mahakama ya kukiondoa mahakamani kielelezo hicho kwa kuwa kilishapokewa mahakamani katika kesi ndogo iliyohusu uhalali wa maelezo ya mshtakiwa wa pili, Adamu Kasekwa.
Akitoa uamuzi, Jaji Tiganga alitupilia mbali mapingamizi hayo akisema mahakama hiyo inao uwezo wa kukipokea kwa kuwa uamuzi uliotolewa awali dhidi ya kielelezo hicho, haukumaliza kesi.
“Mahakama inakuwa Funtus Officio ikithibitika kwamba jambo lililopo mbele ya Mahakama limeshazungumzwa na kutolewa maamuzi. Kwamba jambo hilo linatakiwa liwe limeimaliza kesi kwa kumkuta mshitakiwa ana hatia au kuitisha jambo lolote. Amri hiyo ambayo inakuwa imeinyima Mahakama, inatakiwa iwe na matokeo ya kuifikisha kesi mwisho,” alisema Jaji Tiganga.
Jaji Tiganga alisema; “ukiangalia kimantiki kielelezo ambacho kimetolewa baada ya kielelezo hicho kukataliwa kilikuwa katika suala la utambuzi, na kwamba upokelewaji wake siyo wa mwisho, basi hata kupokelewa kwake siyo jambo la msingi. Hoja ya Funtus Officio naitupilia mbali kwa sababu nilizoeleza.”
Kuhusu hoja ya kutokuwepo kwa amri ya mahakama ya kukitoa kitabu hicho, Jaji Tiganga amesema haina mashiko kwa kuwa msajili wa mahakama anayo mamlaka kufanya hivyo, kwa mujibu wa Mwongozo wa Utunzaji Kilelezo wa 2020.