Waziri wa fedha Dkt.Mwigulu Nchemba akiongea na Vyombo vya habari wakati akielezea mafanikio ya wizara yake katika kipindi Cha miaka 60 ya uhuru wa Tanzania bara
Waziri wa fedha Dkt.Mwigulu Nchemba akiongea na Vyombo vya habari wakati akielezea mafanikio ya wizara yake katika kipindi Cha miaka 60 ya uhuru wa Tanzania bara
**
Na Dotto Kwilasa, Malunde 1 blog Dodoma
WAZIRI wa fedha na mipango Dkt. Mwigulu Nchemba amezitaka Sekta zinazoleta uzalishaji nchini ziendane na mazingira ya sasa ili kuwawezesha watanzania hususani vijana kubadili mfumo wa maisha kwa kukubali kujitoa kufanya kazi kwa bidii ili kuepuka utegemezi kwa Wazee.
Dkt.Nchemba ameyasema hayo leo Jijini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya wizara hiyo katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru na kufafanua kuwa kadri siku zinavyozidi kwenda Wazee wengi nchini wamekuwa wakitwishwa mzigo wa Majukumu na kuwasababishia hofu na magonjwa .
"Lazima kitu kifanyike hapa,vijana wanapaswa kujishighulisha na sio kuwategemea Wazee,lazima tuwe na huruma kwa Wazee wetu,nguvu kazi ikiwa kubwa uzalishaji unaongezeka,kila mtu akijitoa kufanya kazi haya uchumi wetu unakua ,"amesema na kuongeza;
Haiwezeka hadi sasa kipindi ambacho nchi iko katika uchumi wa kati eti bado kuna vijana ukiwauliza mbona sijakuona online anasema sikuwa na bando ,yani hata bando anataka awekewe na baba yake ambaye pengine ni mzee,lazima tubadilike,"amesisitiza
Kadhalika amesema ,Tanzania ikiwa inaadhimisha miaka 60 ya uhuru,pato la Taifa limepungua kasi ya kukua kutoka asilimia 7.0 mwaka 2019 hadi asilimia 4.8 mwaka 2020 kutokana na athari za hatua zilizochukuliwa na mataifa mbalimbali duniani ambao ni washirika wakubwa wa biashara wa Tanzania katika kukabiliana na janga la UVIKO-19.
Amesema miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na mataifa hayo ni pamoja na kufunga mipaka, kusitisha safari za ndege za kimataifa na kusitisha baadhi ya shughuli za kiuchumi zinazohusisha mikusanyiko na kutaja kuwa hatua hizo zilisababisha uchumi wa dunia kuporomoka mwaka 2020 ambapo nchi nyingi zilikuwa na ukuaji hasi na kwa nchi za Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara, ni nchi 11 tu zilikuwa na ukuaji chanya kati ya nchi 45.
Ameelezea mwenendo wa wizara hiyo tangu uhuru na kusema uchumi wa Tanzania ulipitia katika nyakati mbalimbali za mafanikio ya kiuchumi pamoja na changamoto kadhaa zikiwemo ukame katika miaka ya mwanzoni mwa 1970 na 2012, mdororo wa uchumi wa mwaka 2008, vita vya Kagera mwaka 1978 pamoja na ugonjwa wa UVIKO mwaka 2020.
Hata hivyo alieleza kuwa Serikali ya awamu ya sita imeingia madarakani katika kipindi ambacho dunia bado inapambana na athari za kiuchumi na kijamii za janga la UVIKO-19 Katika nusu ya kwanza ya mwaka 2021, (Januari – Juni) uchumi umekua kwa asilimia 4.7 ikilinganishwa na asilimia 5.0 katika kipindi kama hicho mwaka 2020 na kupungua kwa kasi ya ukuaji katika kipindi hicho kumetokana na athari za UVIKO-19 katika shughuli mbalimbali za kiuchumi .
"Kwa sababu hiyo shughuli nyingi za kiuchumi zimeendelea kuwa na viwango chanya vya ukuaji katika nusu ya kwanza ya mwaka 2021 ingawa kasi yake ilipungua ukilinganisha na kipindi kama hicho mwaka 2020,"ameeleza.