Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MIFUGO YATAKIWA KUPATIWA CHANJO ILI KUFIKIA UFUGAJI BORA


Na. Edward Kondela
Chama cha Madaktari wa Wanyama Tanzania (TVA), leo kimezindua kampeni ya kutoa chanjo kwa wanyama wafugwao ili kuikinga dhidi ya magonjwa mbalimbali ikiwa ni sehemu ya mkutano wa 39 wa kisayansi wa chama hicho utakaofanyika jijini Dodoma.

Akizungumza katika Tarafa ya Hombolo iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma Mwenyekiti wa TVA Prof. Esron Karimuribo, wakati akizindua rasmi zoezi hilo ambalo limefanyika pia katika Wilaya ya Chamwino, amesema TVA inaungana na serikali katika kuhimiza wafugaji kote nchini kuitikia wito wa kukabiliana na magonjwa ya wanyama kwa kuipatia chanjo dhidi ya magonjwa mbalimbali.

Amebainisha kuwa katika zoezi hilo chanjo zinazotolewa ni dhidi ya kichaa cha mbwa, pamoja na chanjo za magonjwa 13 ya kipaumbele yaliyoainishwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Pro. Karimuribo ametoa rai kwa wafugaji kuitikia wito wa kutoa chanjo kwa wanyama wanaowafuga katika kutokomeza magonjwa mbalimbali na kufikia dhana ya ufugaji bora pamoja na walaji kula mazao yenye ubora kutoka katika wanyama hao ikiwa ni pamoja na nyama na maziwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari wa Wanyama kutoka nchini Kenya (KVA) Dkt. Nicholas Muyale ambaye ameshiriki pia katika zoezi la utoaji wa chanjo kwa wanyama, amesema utoaji wa chanjo kwa wanyama ni muhimu kwa kuwa unadhibiti magonjwa yanayoweza kuvuka mipaka ya nchi.

Aidha, amesema KVA imekuja kushiriki katika mkutano wa 39 wa kisayansi ulioandaliwa na TVA kwa ajili ya kujifunza kwa pamoja na kushirikiana katika mawazo na sayansi.

Nao baadhi ya wananchi ambao mbwa wao wamepatiwa chanjo dhidi ya ugonjwa wa kichaa, wameshuruku utoaji huo wa chanjo na kwamba watakuwa mabalozi kwa wenzao ili nao waweze kuchanja mifugo yao kwa kuwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa umekuwa ukisababisha madhara makubwa kwa binadamu endapo aking’atwa na mbwa mwenye ugonjwa huo.

Zoezi la utoaji wa chanjo kwa wanyama lililofanyika katika Tarafa ya Hombolo kwenye Halmashauri ya Jiji la Dodoma pamoja na Wilaya ya Chamwino ni sehemu ya mkutano wa 39 wa kisayansi wa Chama cha Madaktari wa Wanyama Tanzania (TVA) unaotarajiwa kufunguliwa kesho (24.11.2021) jijini Dodoma na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki.

Kauli mbiu ya mkutano huo ni “Kuendeleza Afya Moja Katika Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi na Magonjwa ya Mlipuko Katika Kuunga Mkono Uchumi wa Kati na Malengo ya Maendeleo Endelevu.”




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com