RAIS SAMIA : MNAPOVUNA MITI MKUMBUKE NA KUPANDA MINGINE ZAIDI


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza Wana-Iringa na Watanzania kwa ujumla kuwa wahakikishe wakati wanavuna miti wakumbuke na kupanda miti mingi zaidi ili waweze kupata faida zote zinazotokana na maliasili hiyo.

Ameyasema hayo jana (Jumamosi, Novemba 13, 2021) wakati akifungua Kongamano la Uwekezaji kwenye Sekta ya Misitu lilifanyika katika Viwanja vya Wambi vilivyopo Mji Mafinga, Iringa. Mheshimiwa Rais amenituma niwaambie kuwa tunapovuna miti tuhakikishe tunapanda mingine ili kutunza mazingira.”

Pia, Waziri Mkuu ametoa maelekezo mbalimbali kwa ajili ya kuboresha sekta ya misitu ikiwa ni pamoja na kuzielekeza Wizara za Maliasili na Utalii na Wizara ya Viwanda na Biashara ziweke mazingira wezeshi ya kuvutia uanzishaji na uendelezaji wa viwanda vya mazao ya misitu ili kuchakata mazao hayo kwa ufanisi na tija.

“Nitoe wito kwa wawekezaji kuja Iringa na kutumia vema fursa za uwekezaji zilizopo kwenye miradi mikubwa ya mashamba ya miti na viwanda vya mazao ya miti. Viwanda hivyo vitasaidia kuepusha upotevu mwingi wa malighafi na kuwezesha kutumia mabaki yake kuzalisha bidhaa nyingine.”

Mheshimiwa Majaliwa amewaelekeza viongozi wa Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF) waendelee kuwawezesha wajasiriamali wa misitu washiriki katika shughuli za misitu kwa kutoa ruzuku ili kuongeza kipato cha jamii.

Pia, Waziri Mkuu ameuelekeza uongozi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kushirikiana na mamlaka nyingine ikiwemo TAWA kuendeleza utatuzi wa migogoro iliyopo baina ya wananchi na maeneo yaliyohifadhiwa.

“…TFS endeleeni kuimarisha ulinzi na usimamizi wa rasilimali hii kwenye mashamba ya miti, hifadhi za misitu, mapori ya akiba, mapori  na tengefu pamoja na kuhakiki mipaka na kuweka vigingi vinavyoonekana katika maeneo hayo.”

Aidha, Waziri Mkuu ameelekeza Wizara ya Maliasili na Utalii mamlaka iweke mazingira mazuri yatakayowezesha sekta hiyo kuzalisha ajira nyingi zaidi kupitia mazao mbalimbali yatokanayo na maliasili hiyo kama ufugaji wa nyuki.

Mheshimiwa Majaliwa amesema ni muhimu kuendeleza utekelezaji wa mikakati ya kuwanufaisha wananchi wanaoishi jirani na misitu kupitia miradi ya ufugaji nyuki ikiwemo kutoa elimu kwa vikundi vya wafugaji nyuki na mafundi seremala.

Kadhalika, Waziri Mkuu amezielekeza Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Wizara ya Viwanda na Biashara zishirikiane katika kufatuta masoko ya mbao nje ya nchi. “Nendeni mkatafute masoko katika nchi zenye uhitaji.

Mheshimiwa Majaliwa amezielekeza taasisi zinazohusika na masuala ya misitu ziendeleze programu mbalimbali za upandaji miti ili kutunza mazingira na kuongeza kipato kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Majaliwa amemuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Uwekezaji ahakikishe bidhaa zinazozalishwa katika viwanda mbalimbali nchini vikiwemo vya plywood zinawekwa nembo inayoonesha kuwa zimezalishwa nchini. “Lazima bidhaa hizo zioneshe maeneo zilikozalishwa.”

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Geoffrey Mwambe amesema wizara anayoiongoza kwa kushirikiana na wadau wa uwekezaji atahakikisha changamoto zote zinawakabili wawekezaji nchini zinatafutiwa ufumbuzi.

Kwa Upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damas Ndumbaro amsema wizara anayoiongoza imefanikiwa kutatua changamoto mbalimbali zilizokuwa zinaikabili sekta ya misitu ikiwemo ya utoaji wa vibali vya mazao ya misitu.

Amesema Wizara ya Maliasili na Utalii imefanikiwa kurekebisha mikataba ya uvunaji wa mazao ya misitu ambayo ilikuwa ni ya mwaka mmoja na kuwafanya wahusika wakose fursa za mikopo kutoka taasisi za kifedha na sasa inatolewa kwa miaka mitatu.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Queen Sendiga alisema pamoja na mambo mengine kongamano hilo la siku tatu linalenga kuwakutanisha wadau wa sekta ya misitu ili kuongeza thamani katika mazao ya misitu pamoja na kutangaza fursa za uwekezaji kwenye sekta hiyo, hivyo kuongeza tija kwa mkoa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post