Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na mgeni wake Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam leo tarehe 27 Novemba 2021 kwa ajili ya ziara ya Kitaifa ya siku tatu hapa nchini.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiwa na mgeni wake Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni akimtambulisha ujumbe aliofuatana nao mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam leo tarehe 27 Novemba 2021 kwa ajili ya ziara ya Kitaifa ya siku tatu hapa nchini.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiwa na mgeni wake Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni wakisalimiana na Wasanii wa vikundi vya ngoma mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam leo tarehe 27 Novemba 2021 kwa ajili ya ziara ya Kitaifa ya siku tatu hapa nchini.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiwa na mgeni wake Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam leo tarehe 27 Novemba 2021 kwa ajili ya ziara ya Kitaifa ya siku tatu hapa nchini.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa amesimama na mgeni wake Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni wakati nyimbo za mataifa mawili (Tanzania &Uganda na ule wa Afrika Mashariki) zikipigwa katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam leo tarehe 27 Novemba 2021 mara baada ya Rais wa Uganda Mhe. Museveni kuwasili nchini.
Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni, akikagua Gwaride la JWTZ nara baada ya kuwasili katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam leo tarehe 27 Novemba 2021 mara baada ya Rais wa Uganda Mhe. Museveni kuwasili nchini.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na mgeni wake Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni wakati alipowasili katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam leo tarehe 27 Novemba 2021 mara baada ya Rais wa Uganda Mhe. Museveni kuwasili nchini.
**
Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni amewasili nchini kwa Ziara ya Kitaifa ya siku 3 yenye lengo la kuimarisha uhusiano baina ya nchi yake na Tanzania kufuatia mualiko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Jijini Dar es Salaam, Mhe. Rais Museveni amekagua gwaride la heshima lililoandaliwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa ajili yake pamoja na kupigiwa mizinga 21.
Mhe. Rais Museveni alipowasili Ikulu Jijini Dar es Salaam amefanya mazungumzo na mwenyeji wake Mhe. Rais Samia pamoja na kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu masuala mbalimbali ya uhusiano na ushirikiano wa nchi hizi mbili.
Katika mazungumzo yake na vyombo vya habari, Mhe. Rais Samia amesema Tanzania inaridhishwa na uhusiano mzuri na wa kindugu uliopo kati yake na Uganda na kusisitiza kuwa uhusiano huo utaendelea kudumishwa.
Mhe. Rais Samia amesema yeye na Rais Museveni wamewaelekeza Mawaziri wa Kisekta kukutana mara kwa mara kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika maeneo yao ili kuendelea kuimarisha ushirikiano huo.
Pia, Mhe. Rais Samia amesema Uganda ni nchi ya pili kwa uwekezaji hapa nchini kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambapo Uganda imetoa ajira 2,150 kwa watanzania. Mhe. Rais Samia ameahidi kwamba Tanzania itaendelea kuwekeza zaidi nchini Uganda ili kukuza zaidi kiwango cha biashara.
Mhe. Rais Samia amesema kwa lengo la kuimarisha biashara kati ya nchi mbili hizo, wamekubaliana kushughulikia kwa pamoja vikwazo visivyokuwa vya kikodi na kuviondoa.
Amesema, katika mazungumzo yake na Mhe. Rais Museveni wamekubaliana kukuza biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili kwa kuwa bado kuna fursa nyingi za kibiashara hususan katika sekta za viwanda, kilimo, uvuvi, huduma za kijamii, utalii pamoja na usafirishaji.
Vilevile, Mhe. Rais Samia amemshukuru Mhe. Rais Museveni pamoja na Serikali ya Uganda kwa uamuzi wa kuendelea kutumia Bandari ya Dar es Salaam kupitisha shehena mbalimbali za mizigo ikiwemo itakayotumika katika ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi mkoani Tanga nchini Tanzania.
Mhe. Rais Samia pia amemuomba Mhe. Rais Museveni kuridhia Mamlaka ya Bandari nchini kufungua ofisi yake ya uratibu Jijini Kampala, Uganda kwa ajili ya kusogeza karibu huduma za Bandari kwa wateja waliopo Uganda.
Aidha, Mhe. Rais Samia amesema Serikali ya Tanzania na Uganda zimekubaliana kujenga viwanda vya kutengeneza chanjo ya UVIKO 19 pamoja na magonjwa mengine ikiwa ni jitihada za kupambana na kuenea kwa magonjwa hayo.
Mhe. Rais Samia amemshukuru Mhe. Rais Museveni kwa uamuzi wa kujenga Shule ya Msingi Museveni yenye Mtaala wa Kiingereza wilayani Chato mkoani Geita na kueleza kuwa hatua hiyo ni ishara ya upendo, undugu na uhusiano mzuri kati ya nchi hizo mbili.
Kwa upande wake Mhe. Rais Museveni amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa mualiko wa kuja kutembelea Tanzania katika ziara hiyo ambayo amesema inazidi kuimarisha uhusiano wa kindugu baina ya mataifa hayo uliokuwepo kwa muda mrefu.
Mhe. Rais Museveni amesema wamekubaliana kuwa Serikali zote mbili zitaendelea kusimamia mradi wa ujenzi wa Bomba la kusafirisha mafuta ghafi la Afrika Mashariki kutoka Hoima Uganda hadi Tanga nchini Tanzania na kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kuleta manufaa yaliyokusudiwa.
Jaffar Haniu
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.