REA YAVUKA MALENGO KUWAFIKIA WANANCHI VIJIJINI

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy (katikati) akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za Wizara ya Nishati leo Novemba 30,2021 Jijini Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy akisisitiza jambo mbele ya waandishi wa habari katika Ofisi za Wizara ya Nishati leo Novemba 30,2021 Jijini Dar es Salaam.Kamishna Msaidizi wa umeme, Wizara ya Nishati, Mhandisi Styden Rwebangila akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za Wizara ya Nishati leo Novemba 30,2021 Jijini Dar es Salaam.

(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)

*************************

Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imesema imevuka malengo iliyojiwekea ya asilimia 50 katika kuwafikishia wananchi huduma ya umeme viijini ambapo hadi kufikia Juni 2021 asilimia 69.6 ya vijiji vilikuwa vimefikiwa na huduma hiyo.

Akiongea leo Novemba 30, 2021 katika ukumbi wa Wizara ya Nishati Jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa REA Mhandisi Hassan Seif Saidy alisema kuwa wakati Taifa linaelekea kuadhimisha miaka 60 ya uhuru, hali ya maisha ya wakazi wa vijijini imebadilika ambapo mwaka 2007 wakati Wakala inaanzishwa asilimia 2 tu ya vijiji walikuwa wamefikiwa na huduma ya umeme.

“ Kuna mafanikio mengi tuliyoyapata kutokana na usanifu, utekelezaji na usimamizi wa miradi inayotekelezwa na wakala tangu kuanziswa kwake ambapo miradi hiyo imewezesha ujenzi wa jumla ya kilomita 38,296.56 za umeme msongo wa kati na kilomita 35,253.43 za umeme msongo mdogo lakini pia kuna jumla ya wateja 716,847 waliounganishiwa umeme kwa gharama ya shilingi bilioni 2,661.93 kwa kipindi cha miaka 14 tangu kuanzishwa kwake”, alisema Mhandisi Saidy.

Mafanikio mengine yaliyopatikana ni pamoja na kutengeneza masoko kwa viwanda vya ndani vinavyozalisha vifaa vinavyotumika katika ujenzi wa miradi ya umeme, kuwezesha uboreshwaji wa kilimo cha umwagiliaji katika mashamba likiwemo shamba la Mtakuja Kilimanjaro na Zuzu Dodoma.

Aidha, kufunga mifumo ya umeme katika nyumba za wafanyakazi takribani 831 kwenye sekta ya afya na elimu katika mikoa ya Shinyanga, Kigoma, Kagera, Pwani, Lindi, Mtwara, Ruvuma na Tabora, wakati huo huo hali ya kuboresha mazingira ya makazi vijijini ambayo imepelekea kupunguza uhamiaji wa vijana kutoka vijijini kwenda mjini kwa kuwa umeme umewamewezesha kufanya shughuli za kiuchumi kwenye makazi yao.

“ Vijana wengi sasa wanatulia vijijini kwani wameweza kuanzisha viwanda vidogo na vya kati katika juhudi za kujikwamua kiuchumi. Vitu kama vile mashine za kusaga, kuchomelea, viwanda vya uselemara pamoja na saloni za kike na kiume vinapatikana hadi vijijini siku hizi, lakini pia upatikanaji wa taarifa na burudani kwa wepesi kama vile televisheni na redio vimeongeza utulivu kwa vijana wengi hapa nchini”, aliongeza.

Kwa upande wake kamishna Msaidizi wa umeme, Wizara ya Nishati, Mhandisi Styden Rwebangila alisema kwamba katika kuhakikisha mtu mmoja mmoja anafaidika na uwepo wa umeme, Serikli inahamasisha wananchi wengi waone umuhimu wa kuunganishiwa umeme kwenye makazi yao ili kufaidi fursa zinazoletwa na nishati hiyo.

“ Tunaondoka kwenye hatua ya kuhakikisha umeme unafika kijijini, na hivi sasa tunawahamiasisha wakazi wa eneo husika kuhamasika kuunganishiwa umeme huo kwenye makazi yao. Mwamko ni mkubwa na tunapokea maombi mengi na hivi sasa tunahamasisha ushiriki wa sekta binafsi, taasisi za fedha katika uwekezaji wa miradi ya Nishati vijijini na tunaendelea kuhamasisha utekelezaji wa miradi ya nishati jadidifu kutoka vyanzo vya asili vinavyopatikana maeneo ya vijijini na kwenye visiwa”, alisema Mhandisi Rwebangila.

Wakala wa Nishati Vijiji ulianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Nishati vijijini Na. 8 ya mwaka 2005 na kuanza rasmi utekelezaji wa majukumu yake mwezi Oktoba, 2007 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa iliyokua Sera ya Taifa ya Nishati ya mwaka 2003.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post