SERIKALI YAIPA HALMASHAURI HANANG USIMAMIZI SHAMBA LA NGANO


Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto akipitia nyaraka za makabidhiano ya Mali za Shamba la Ngano la Basotu lililopo wilayani Hanang wakati wa tukio la makabidhiano ya mali za shamba hilo kutoka kwa Mfilisi, Kampuni ya Uwakili ya Tadayo. Hafla fupi ya makabidhiano hayo ilifanyika jana katika Ofisi za Msajili wa Hazina jijini Dar es Salaam.(Picha na Ofisi ya Msajili wa Hazina)


Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto (kushoto) na Wakili Joseph Tadayo kutoka Kampuni ya Uwakili ya Tadayo wakisaini hati ya makabidhiano ya Mali za Shamba la Ngano la Basotu lililopo wilayani Hanang wakati wa tukio la makabidhiano ya mali za shamba hilo kutoka kwa Mfilisi, Kampuni ya Uwakili ya Tadayo. Hafla fupi ya makabidhiano hayo ilifanyika jana katika Ofisi za Msajili wa Hazina jijini Dar es Salaam.(Picha na Ofisi ya Msajili wa Hazina)


Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto akipokea hati ya makabidhiano ya Mali za Shamba la Ngano la Basotu liliopo wilayani Hanang kutoka kwa Wakili Joseph Tadayo wa Kampuni ya Uwakili ya Tadayo wakati wa tukio la makabidhiano ya mali za shamba hilo kutoka kwa Mfilisi, Kampuni ya Uwakili ya Tadayo. Hafla fupi ya makabidhiano hayo ilifanyika jana katika Ofisi za Msajili wa Hazina jijini Dar es Salaam.(Picha na Ofisi ya Msajili wa Hazina)


Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto akikabidhi kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Jenifa Omolo hati ya uangalizi wa mali za shamba la ngano la Basotu wilayani humo katika Ofisi za Msajili wa Hazina jijini Dar es Salaam, jana. Kwa muda mrefu, mali za shamba hilo zilikuwa chini ya uangalizi wa Mfilisi, Kampuni ya Uwakili ya Tadayo inayoongozwa na Wakili Joseph Tadayo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mwanga mkoani Kilimanjaro. Hafla fupi ya makabidhiano hayo ilifanyika jana katika Ofisi za Msajili wa Hazina jijini Dar es Salaam.(Picha na Ofisi ya Msajili wa Hazina)

****************************

Na Mwandishi Maalumu

SERIKALI imeikabidhi Halmashauri ya wilaya ya Hanang usimamizi na uangalizi wa muda wa mali zote zilizopo katika shamba la ngano la Basotu wilayani humo lenye ukubwa wa hekta 5,138 wakati Serikali ikiandaa mipango ya muda mrefu ya matumizi ya shamba hilo.

Hatua hiyo imekuja baada ya mali katika shamba hilo kuwa chini ya uangalizi wa Mfilisi, Kampuni ya Uwakili ya Tadayo kwa zaidi ya miaka 15. Mwaka 2004, Mfilisi, Wakili Joseph Tadayo, Mbunge wa sasa wa Jimbo la Mwanga, alikabidhiwa kwa ajili ya kuuza shamba na mali zake, lakini baadaye mwaka 2007, Serikali ilisitisha uamuzi huo na kuziacha mali hizo chini ya uagalizi wa Kampuni ya Uwakili ya Tadayo.

Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto jana alipokea mali za shamba hilo la Basotu kutoka kwa Mfilisi, Wakili Joseph Tadayo, makabidhiano yaliyofanyika katika Ofisi za Msajili wa Hazina, jijini Dar es Salaam.

“Ofisi yangu inashukuru kwa kazi ya uangalizi iliyofanywa na Kampuni ya Tadayo licha ya kuwepo kwa changamoyo kadhaa,” alisema Msajili wa Hazina mara baada ya kupokea hati ya makabidhiano.

Hati hizo zinaonesha kuwepo kwa mali mbalimbali katika shamba hilo zikijumuisha mitambo na majengo 37, zikiwemo nyumba za makazi 28, maghala mawili, vihenge (silos) sita, ukumbi wa starehe, mgahawa, kanisa, duka na mitambo mbalimbali pamoja na matrekta na mashine za kuvunia nafaka.

Mara baada ya kukabidhiwa hati za mali ya shamba hilo, Mgonya alizikabidhi kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Hanang, Jenifa Omolo kwa ajili ya uangalizi wa muda wakati serikali ikamilisha mpango wa matumizi wa muda mrefu wa shamba hilo.

“Kwa upande wa Halmashauri, Ofisi yangu inashukuru uongozi wa Halmashauri ya Hanang kwa ushirikiano mkubwa ambapo imekuwa ikitupatia na leo hii tunaiongezea jukumu lingine la uangalizi wa mali mpaka hapo maelekezo mengine ya Serikali yatakapotolewa,” alisema Mgonya, huku Mkurugenzi wa Halmashauri ya Hanang akiahidi kutimiza wajibu wake ili kulinda mali hizo za Serikali.

Naye Wakili Tadayo aliyekuwa Mfilisi wa Shamba la Basotu, alisema amekuwa mwenye furaha kukabidhi mali hizo, baada ya kuwa mwangalizi kwa muda mrefu, huku akikabiliana na changamoto kadhaa.



Shamba la Basotu ni kati ya mashamba saba ya ngano ya Serikali wilayani Hanang yaliyokuwa chini ya Shirika la Taifa la Kilimo na Chakula (NAFCO). Aidha, ni Shamba pekee ambalo halikubinafsishwa baada ya Serikali kusitisha uamuzi huo mwaka 2007. Kutokana na kukaa muda mrefu bila kubinafsishwa, kuliibuka vitendo vya uvamizi kutoka kwa wakulima na wafugaji wa maeneo jirani, hali iliyoilazimu Halmashauri Kuiomba Ofisi ya Msajili wa Hazina iridhie shamba hilo liwekwe chini ya usimamizi wao ili kuzuia vitendo vya uvamizi wa shamba na wizi wa mali.

Mashamba mengine ni Gawal, Warret, Gidagamowd, Satchet, Murjanda na Mulbadaw. Mashamba ya Gawal na Warret yalikabidhiwa kwa Halmashauri ya wilaya na kugawiwa wananchi kwa matumizi ya kilimo, ufugaji na makazi, na mashamba ya Gidagamowd, Satchet na Murjanda yalibinafsishwa kwa Kampuni ya Ngano Limited mwaka 2005. Shamba la Mulbadaw liliuzwa kwa Haydom Lutheran Hospital mwaka 2006.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post