Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SUALA LA MABADILIKO YA TABIANCHI SIYO LA KUFIKIRIKA TENA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Selemani Jafo akiongoza zoezi la upandaji miti kwenye mbio za kuhamasisha utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti ili kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi, zilizofanyika katika viwanja vya Green Oysterbay Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Selemani Jafo (kutoka kushoto) akiwa na Meneja wa Kanda ya Mashariki Kaskazini kutoka NEMC wakimaliza mbio za kilomita 5 za kuhamasisha upandaji miti ili kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi zilizofanyika kwenye viwanja vya Green Oysterbay Jijini Dar es Salaam.

Watumishi walioshiriki mbio za kuhamaisisha upandaji miti “MAZINGIRA MARATHON” kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kumaliza kukimbia kilomita 5.

*******************************

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Selemani Jafo amesema suala la Mabadiliko ya Tabianchi lipo na madhara yake yanaonekana katika sehemu mbalimbali kwenye Nchi yetu ya Tanzania.

Ameyasema hayo wakati wa mbio za kuhamasisha utunzaji wa mazingira (MAZINGIRA MARATHON) zilizofanyika kwenye viwanja vya Green Oysterbay Jijini Dar es Salaam. Mbio hizo zililenga kuhamasisha utunzaji wa mazingira kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi.

Mhe. Jafo amesema dunia kwa sasa ipo hatarini kutokana na mabadiliko ya Tabianchi na kuna baadhi ya maeneo yamesha athiriwa na athari za mabadiliko hayo kama kutoweka kwa Kisiwa cha Kifungu.

Mhe. Jafo ameongeza kuwa kina cha maji kinazidi kuongezeka mfano kwenye visiwa vya Pemba hali inayopelekea uwekezaji kupungua na baadhi ya makazi ya watu hayatakuwepo tena.

Kwa upande wa maziwa Tanganyika na Ziwa Viktoria vina vya maji pia vimeongezeka jambo ambalo linapelekea kuharibika kwa miundombinu na kupoteza uwekezaji uliokuwa karibu na fukwe za maziwa haya.

Aidha Mhe. Jafo ametoa wito kwa Watanzania kuwa na desturi ya kupanda miti ili kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi.

Nae Meneja wa Kanda ya Mashariki Kaskazini NEMC Bw. Anorld Mapinduzi amesema ushiriki wa NEMC kwenye mbio hizo ni sehemu ya kuhamasisha utunzaji wa mazingira sambamba na kufanya mazoezi kwa kuweka afya ya mwili vizuri.

"Tunapozungumzia mazingira tuna maanisha Afya na mazingira endelevu, mambo haya mawili huwezi kuyatenganisha. Huwezi kuwa na afya nzuri kama hutunzi mazingira unayoishi, mfano ikiwa utakata miti huwezi kupata hewa safi na salama na afya itakuwa hatarini".

Bw. Mapinduzi amesisitiza zaidi suala la upandaji miti ili izalishe hewa hewa ya Oksijeni ambayo ni muhimu katika mfumo wa upumuaji, vile vile miti inasaidia kufyonza hewa ya ukaa ambayo inazalishwa na viwanda vyetu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com