Kufuatia joto kali linaloendelea katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania, wataalamu wa Afya, Usalama na Mazingira (HSE) wametoa ushauri wa tahadhari kwamba katika kipindi hiki, wanyama wanaotambaa wakiwemo nyoka na nge wenye sumu kali, hupenda kujificha katika maeneo yenye baridi ndani ya nyumba na makazi ya watu.
Wataalamu hao, wanapendekeza kila mtu kuchukua tahadhari za kuzuia makazi yao kuvamiwa na nyoka na nge kwa kufuata vidokezo na hatua zifuatazo:
- Jambo la kwanza, inashauriwa kuepuka tabia ya kuacha madirisha wazi kwa muda mrefu kwani jamii za nyoka kama Cobra, wanaweza kupanda kwenye ukuta umbali mrefu na kuingia ndani.
- Jambo la pili, ni kuepuka kuacha wazi milango ya mbele ya nyumba kwa nia ya kupata hewa safi hasa nyakati za jioni. Inaelezwa kwamba nyoka wana kawaida ya kutambaa kimyakimya na kuingia ndani endapo wakikuta milango ipo wazi.
- Inashauriwa pia kabla ya kukaa chini ya miti yenye vivuli nyakati za mchana wa jua kali, ni vyema kukagua eneo husika kwani nyoka nao hufuata vivuli na kujificha kwenye matawi ya miti au majani.
- Jambo la nne, unashauriwa kuwa na kawaida ya kukagua kitanda chako kabla ya kulala kwani kuna aina za nyoka wakiwemo Cobra ambao hupenda kujificha chini ya mashuka.
- Unashauriwa kuepuka mtindo wa kulala nje ya nyumba kwa kutandika jamvi au godoro hususan nyakati za jioni kwani nyoka wanaweza kutambaa na kukufikia kwa urahisi.
- Jambo la sita, unashauriwa kufyeka vichaka vinavyozunguka nyumba kwani vichaka hivyo hupendwa na panya ambao ni chakula kikubwa cha nyoka. Unapoacha panya wazagae kwenye makazi yako, utawakaribisha nyoka ambao hupenda kuwinda panya.
- Unashauriwa kutumia dawa maalum ukiwemo unga wa kufukuza nyoka ambao unatakiwa kuunyunyizia kuzunguka makazi yako ili kuwafukuza nyoka.
- Jambo jingine, unashauriwa kuwa makini unapomuona nyoka na kutaka kumuua. Baadhi ya nyoka, huwa na mate yenye sumu ambayo yanaweza kukudhuru hata ukiwa mbali. Pia nyoka aina ya hongo (Black mamba) hupandwa na hasira unapojaribu kuwaua na kuanza kukukimbiza. Unashauriwa kuua nyoka kwa kutumia magongo marefu au mawe kwa kupiga eneo la kichwani bila kukosa.
- Endapo ukiumwa na nyoka kwa bahati mbaya, unashauriwa kujifanyia huduma ya kwanza haraka ikiwa ni pamoja na kufunga eneo la juu ya jeraha la kuumwa na nyoka, kutumia mawe maalum ya kufyonza sumu ya nyoka na kuwahi hospitali haraka iwezekanavyo.
Social Plugin