TANZANIA YASHIRIKI MKUTANO JUKWAA LA USHIRIKIANO KATI YA CHINA NA AFRIKA


Na mwandishi wetu, Dakar

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inashiriki Mkutano wa Nane wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) ulioanza tarehe 28 hadi 30 Novemba 2021 jijini Dakar nchini Senegal.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) ataongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo.

Katika Ufunguzi wa Mkutano wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika, Marais wa Nchi Wenyeviti Wenza wa Mkutano huo Rais wa Jamhuri ya Senegal Mhe. Macky Sall na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Xi Jinping watahutubia Mkutano huo.

Mkutano huo wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika unatanguliwa na Mkutano wa Maafisa Waandamizi unaoanza leo tarehe 28 Novemba 2021 hapa Jijini Dakar, Senegal ambapo Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mpango Zanzibar Dkt. Juma Akil na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bibi Amina Shaaban watashiriki.

Mkutano huo utakaowashirikisha viongozi na wawakilishi kutoka nchi za Bara la Afrika na Jamhuri ya Watu wa China pamoja na mambo mengine utajikita katika majadiliano ya maeneo yafuatayo:- Ushirikiano wa Kisiasa, Ushirikiano wa Kiuchumi, Ushirikiano wa Maendeleo ya Kijamii, Utamaduni na Ushirikiano kati ya Watu na Watu, Ushirikiano wa Ulinzi na Usalama, Mapinduzi ya Kijani, Ubadilishanaji Uzoefu katika masuala ya Uongozi Bora pamoja na Maendeleo ya Kitaasisi ya Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post