Katibu tawala msaidizi uchumi, uzalishaji, uwekezaji,viwanda na Biashara Bi.Aziza Mumba akifungua mafunzo kwa wasindikaji wa zabibu na bidhaa za zabibu jijini dodoma.
Kaimu Mkuu kitengo cha mafunzo Bi.Prisca Stambuli Kisella akitoa mafunzo kuhusu kanuni bora za usindikaji kwa wakulima na wasindikaji wa zao la zabibu eneo la Dodoma . TBS imefanya mafunzo kwa wadau wa zabibu jijini Dodoma katika maeneo ya Dodoma mjini,Hombolo na Mpunguzi.
Meneja wa kanda ya kati wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Bw.Nickonia Mwabuka akiongea na washiriki wa mafunzo kwa wasindikaji wakulima wa zabibu na bidhaa za zabibu jijini Dodoma .
Baadhi ya washiriki wa mafunzo kwa wasindikaji na wakulima wa zao la zabibu jijini Dodoma .
********************
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAKULIMA, wasindikaji wa zao la zabibu katika Mkoa wa Dodoma zaidi ya 100 wamepatiwa mafunzo yanayolenga kuwaelimisha wadau wote waliopo kwenye mnyororo huo kuongeza thamani ya zao hilo ili waweze kuondokana na changamoto mbalimbali.
Mafunzo hayo yaliyoanza kutolewa Novemba 15 na kumalizika Novemba 23, mwaka huu na maofisa wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) katika maeneo matatu ambayo ni Dodoma mjini,Hombolo na Mpunguzi Jiji la Dodoma.
Meneja wa Kanda ya kati,Bw. Nickonia Mwabuka alisema leo wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo kwamba mafunzo hayo yametolewa Dodoma Mjini, Hombolo na Mpunguzi.
Kwa mujibu wa Mwabuka mafunzo hayo yalihusu viwango na matakwa ya viwango vya zabibu na bidhaa za zabibu, kanuni za kilimo bora, kanuni bora za usindikaji na usafi, teknolojia mbalimbali za usindikaji zabibu na bidhaa za zabibu, usajili wa biashara, ufungashaji na vifungashio pamoja na utaratibu wa kuthibitisha ubora wa bidhaa na ushauri kuhusu usafirishaji wa bidhaa kwenda nje ya nchi kuhusiana na masuala ya viwango na ubora.
Alisema mafunzo hayo yametolewa Dodoma kwa kuzingatia kuwa mkoa huo, ndiyo unaolima zao hilo kwa wingi nchini na katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Alifafanua kwamba walengwa wa mafunzo hayo ni wale ambao wapo kwenye mnyororo, yaani wakulima, wasindikaji, wafungashaji wadau wengine ambao wengi ni wajasiriamali wadogo na kati.
"Kundi hili ni sehemu muhimu sana katika sekta hii pamoja na sekta binafsi katika kuchangia pato la taifa, kuongeza ajira na kuondoa umaskini katika nchi yetu,"alisema Mwabuka."
Mwabuka alisema mafunzo hayo yamepokelewa kwa mikono miwili na washiriki wa mafunzo hayo, kwani ni mwanzo wa wadau wa zabibu kuwa na mwelekeo mpya na unaozingatia matakwa ya viwango.
Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka, Katibu Tawala msaidizi Uchumi,uzalishaji, uwekezaji Viwanda na Biashara Bi.Aziza Mumba alisema Serikali ya Awamu ya Tano kupitia tamko la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Julai 5, mwaka huu Serikaii imedhamiria kuliongezea thamani zao la zabibu kuwa miongoni mwa mazao ya kimkakati ili na kuongeza tija kwa wakulima.
Alifafanua kwamba Mkoa wa Dodoma ni mkoa ambao wakazi wake wanalima sana zao la zabibu, lakini wanazo changamoto nyingi ikiwemo kuendelea kuuza zabibu ghafi na ambayo haijafungashwa, kukosa vifungashio vyenye ubora kwa ajili ya kufungasha bidhaa zao.
Mwakilishi huyo wa Mtaka, alitaja changamoto zingine kuwa kukosa elimu juu ya viwango, matakwa ya viwango, kanuni bora za usindikaji, teknolojia ya usindikaji, upatikanaji wa masoko na nyinginezo.
Alisema Serikali inafahamu yote hayo ndiyo maana ilizielekeza taasisi zake zenye mchango katika zao la zabibu kuhakikisha kuwa zinatatua changamoto hizo haraka iwezekanavyo.
Alifafanua kuwa azma ya Serikali ni kuhakikisha inaongeza thamani kwenye zao la zabibu na kuacha kuuza zabibu ghafi kama ilivyo kwa sasa..
"Huku kutafanya nchi yetu kuendelea kujenga uchumi wenye nguvu, imara na wenye ushindani," alisema Mtaka.
Alisema uongozi wa mkoa unaamini kuwa mafunzo haya ni njia muafaka ya kuleta tija zaidi, vile vile kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha sekta ya zao la zabibu na bidhaa zake inakuwa na mchango katika pato la mtu mmoja mmoja pamoja na taifa letu kwa ujumla
"Hii ni kutokana na fursa zilizopo hasa kwenye sekta hii ikiwemo masoko ndani ya nchi yetu na kikanda, ikumbukwe nchi yetu ni nchi mwanachama katika Jumuiya ya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Tunafahamu kuwa baadhi ya nchi wanachama na majirani zetu hawalimi zao la zabibu, hivyo kwetu ni fursa, tuchangamkie.
Social Plugin