Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC), limepokea vichwa vitatu vya treni ya reli ya kati (MGR), vilivyonunuliwa na Serikali kupitia mradi wa uboreshaji wa reli hiyo kwa gharama ya shilingi Bilioni 22.
Ununuzi wa vichwa hivyo ni moja ya mkakati ya Serikali katika uboreshaji wa miundombinu ya Reli hapa nchini (Tanzania Intermodal and Rail Development – TIRP), unaotekelezwa kwa kutumia fedha za mkopo wa Benki ya Dunia.
Vichwa hivyo vilivyopokelewa katika Bandari ya Dar es Salaam na kushuhudiwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, vina lengo la kuongeza tija ya uzalishaji wa Shirika hilo katika usafirishaji wa mizigo kutoka bandarini ya Dar es Salaam hadi Bandari Kavu ya Isaka.
Waziri Prof. Mbarawa, amelitaka Shirika hilo kufanya biashara na kutumia watalaam wenye sifa na uwezo wa kuviendesha vichwa hivyo ili kuweza kusafirisha tani 7,000 mpaka 10,000 za mizigo kwa mwezi na hivyo kuongeza ufanisi wa ubebaji mizigo mara mbili zaidi ya vichwa vilivyopo sasa.
“Nitashangaa sana vichwa hivi wapewe watu ambao hawana sifa na uwezo wa kuviendesha kibiashara kwani kufanya hivyo mtakuwa mmeikosea sana Serikali”, amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Aidha Prof. Mbarawa, amefafanua kuwa kupitia vichwa hivyo gharama za uendeshaji zitapungua lakini pia itapunguza muda wa mizigo kukaa bandarini bila ya kusafirishwa hali inayopelekea msongamano bandarini.
Ameongeza kuwa kuimarika kwa huduma za bandari hapa nchini kumepelekea kuongezeka kwa mizigo inayopita Bandari ya Dar es Salaam hivyo mahitaji ya behewa na vichwa vya treni kwa ajili ya kuhudumia wateja wa nje na ndani ya nchi kwasasa umeongezeka.
Amesema vichwa hivyo vina uwezo wa Horse Power 3,000 kwa kila kimoja kwa ajili ya kuvuta behewa 20 ambazo ni sawa na tani 1,200 kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro tofauti na awali ambapo vilikuwa vikifungwa vichwa viwili.
Prof. Mbarawa amefafanua kuwa usafirishaji wa mizigo kwa njia ya reli utapunguza uharibifu wa barabara zetu hapa nchini kwa kiasi kikubwa.
Awali akitoa taarifa ya vichwa hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la TRC Bw. Masanja Kadogosa, ameeleza kuwa mkataba wa ununuzi wa vichwa vitatu ulisainiwa tarehe 4 Machi 2019 katika shirika hilo na kampuni ya SMH RAIL kutoka nchini Malaysia kwa mkataba wa siku 360.
Bw. Kadogosa amefafanua kuwa kichwa kimoja cha reli hiyo ya kati kitaongezewa mzigo hadi kufikia tani 2,000 ambazo ni sawa na behewa 33 ambapo mzigo huo ukisafirishwa kwa njia ya barabara ni sawa na malori 66 yenye uwezo wa kubeba tani 30 kila moja.
Ameongeza kuwa vichwa hivyo vipya vimefungwa mifumo ya kisasa ambayo itasaidia kuongeza ufanisi na uimarishaji wa usalama wa safari za treni.
“Treni hii imefungwa kifaa cha kutoa taarifa kwa waongoza treni kwa njia ya mtandao ili kuweza kufatilia mwenendo wa safari kuanzia Dar es Salaam hadi mwisho wa safari lakini pia katika taarifa zitazopatikana ni pamoja na mwendokasi wa treni, aina treni, matumizi ya mafuta, mahali treni ilipo na hitilafu ya kichwa cha treni pindi inapopata shida ili kupata ufumbuzi wa haraka”, amefafanua Bw. Kadogosa.
Mradi wa ununuzi wa vichwa vitatu vya treni za reli ya kati kutalifanya Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuwa na jumla ya vichwa vya treni 43 vya masafa marefu na vichwa vya sogeza 7 katika uendeshaji wake.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin