Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro amewataka Wadau wa sekta ya Utalii nchini kuungana na Serikali katika vita dhidi ya ujangili pamoja na uvamizi wa maeneo yaliyohifadhiwa baadala ya kuiachia Serikali pekee
Ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki mkoani Ruvuma mara baada ya kufanya doria kwa kutumia ndege ndogo katika maeneo yaliyohifadhiwa na kujionea uharibifu mkubwa unaoendelea kufanywa na Wavamizi wakiwemo wakulima na wafugaji.
Amewataja wadau hao kuwa ni Chama cha Wasafirishaji wa Watalii ( TATO), Chama cha Mahotelia ( HAT) Chama cha Wawindaji wa Kitalii ( TAHOA) Shirikisho la Vyama vya Utalii nchini ( TCT ) pamoja Chama cha Waongoza Wataii ( TTGA)
Katika doria hiyo, Dkt.Damas Ndumbaro aliongozana na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa mkoa wa Ruvuma pamoja na Mkuu wa mkoa huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama wa mkoa huo, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge
Kwa mujibu wa takwimu sekta ya Utalii nchini inategemea zaidi ya asilimia 80 ya utalii wa wanyamapori
Kufuatia takwimu hizo, Dkt.Ndumbaro amesema kutokana na kasi ya Wafugaji kuingiza mifugo na huku Wakulima kuendelea kulima ndani ya maeneo ya Hifadhi kunatishia kupungua au kuisha kabisa kwa Wanyamapori ambao watalii hutoa pesa nyingi kuja nchini kwa ajili ya kuwaona
Amesema katika vita ya kupambana na Wavamizi katika maeneo ya Hifadhi hususan Wafugaji kunahitaji ushirikiano mkubwa kutoka Sekta binafsi kwani Wafugaji ni watu wenye ushawishi mkubwa katika jamii, watoa rushwa na wanakikundi cha Wanasiasa wakiwemo wabunge wanaowatetea pindi wanapokamatwa wakiwa wameingiza mifugo katika maeneo ya Hifadhi.
" Ili muendelee na biashara za utalii nchini sisi kama Serikali pamoja na ninyi Wadau wa Utalii ni lazima tuzungumze lugha moja tuwakemee wale wote ambao hawautakii mema uhifadhi, huwautakii mema utalii wetu, hawautakii mema uchumi wetu," alisisitiza Ndumbaro.
Amesisitiza kuwa kama Wadau wa Utalii nchini wataendelea kuitegemea serikali pekee ndiyo yenye jukumu la kulinda maeneo yaliyohifadhiwa, itafika muda watalii wataacha kuja nchini kwani maeneo yote yaliyohifadhiwa yatakuwa yamejaa mifugo pamoja na mashamba ya mazao badaala ya wanyamapori.
" Nawasihi Wadau wote wa utalii nchini pazeni sauti zenu , naamini sauti zenu zina nguvu sana waambieni Wafugaji hili suala la kuingiza mifugo hifadhini kwa kisingizio kuwa hakuna maeneo ya malisho halikubaliki hata kidogo" alisisitiza Dkt.Ndumbaro
Amefafanua kuwa ili Wadau wa utalii nchini waendelea kufanya biashara zao katika sekta ya utalii wanategemea sana uimara wa maeneo yaliyohifadhiwa kutokana na uvamizi mkubwa unaoendelea serikali ni lazima ishirikiane na Wadau hao katika kupambana na Wavamizi hao.
Amewatahadhalisha Wadau hao kuwa kama wataendelea kukaa pembeni na kunyamazia wafugaji kuingiza mifugo yao basi biashara ya utalii nchini ipo hatarini kutoweka na watu zaidi milioni 1.5 walioajiriwa katika sekta hiyo watapoteza ajira zao kwani kutokana na uvamizi pamoja na ujangili wanyamapori wanazidi kupungua siku hadi siku.
Katika hatua nyingine, Dkt.Ndumbaro amesema kumeibuka aina mpya ya majangili ambao hujidai kama wachungaji kwa kuingiza mifugo maeneo ya Hifadhi lakini hubeba bunduki kwa ajili ya kuua wanyamapori
Kufuatia hali hiyo, Dkt.Ndumbaro amesewatahadharisha Wadau wa Utali nchini wasifikirie kuwa wapo salama kwani uchumi wao unawategemea sana watalii bila kuungana na serikali kupaza sauti na kukemea Wafugaji wanaoingiza mifugo ndani ya Hifadhi uchumi wao utakuwa matatani siku za usoni
Akizungumzia maeneo aliyofanya doria kwa kutumia ndege, Dkt.Ndumbaro amesema hali ni mbaya wafugaji wameokana wakiwa na maelfu ya ng'ombe katikati ya maeneo ya Hifadhi huku wakulima wakiwa katikati ya maeneo ya Hifadhi wameonekana wakilima katika vyanzo vya maji huku wakiwa wakikata miti kwa kasi pamoja na wachimba madini wakiwa wamevamia maeneo hayo hali ambayo sio salama kwa Wanyamapori
Akitaja maeneo yaliyofanyiwa doria kuwa ni Pori la Akiba la Selous, Hifadhi ya Wanyamapori ya Jamii ya Mbalang'andu, Pori la Akiba la Litambyandosi pamoja na Pori la Akiba la Liparamba.
Naye, Mkuu wa mkoa wa Ruvuma pamoja na Mkuu wa mkoa huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama wa mkoa huo, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amesema Wafugaji ni lazima wapeleke mifugo yao katika maeneo yaliyopangwa na sio kuvamia maeneo ya hifadhi huku akiwaonya wakulima kuacha kuvamia maeneo ya hifadhi kwani ni hatari kwa ajili ya maisha yao
Amewataka wavamizi wote wajiandae kuondoka mara moja kabla ya kusbiri kuanza kuondolewa.