Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DKT. GWAJIMA : WIZARA, MSALABA MWEKUNDU TUSHIRIKIANE


Na Majid ABDULKARIM, WAMJW- DSM
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima amewataka watumishi wa Wizara yake kutoa Ushirikiano ulioimarika kwa taasisi ya Msalaba Mwekundu na kuja na mkakati wa ushirikiano baina ya pande hizo mbili kwa maslahi mapana ya Jamii.

Dkt. Gwajima ameyasema hayo  tarehe 17 Novemba, 2021 alipotembelea Makao Makuu ya Taasisi hiyo Jijini Dar es Salaam.

Amesema, ipo haja ya kuimarisha ushirikiano baina ya pande zote na kuwa na mkataba rasmi wa mashirikiano Ili kuongeza Kasi ya taasisi hizi kufikisha huduma za kijamii kwa wakati na ubora.

“shirikianeni ili muweze kuja na mpango huo haraka tukianza mwaka mpya tuwe na utaratibu mzuri na rasmi wa ushirikiano” Amesema Dkt. Gwajima

Kwa upande wake Rais wa Shirika hili la kimataifa la Msalaba mwekundu hapa nchini Mhe. David Kihenzile ameiomba wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na watoto kuijengea uwezo taasisi hiyo ikiwa ni pamoja na kuipa kipaumbele pale inapohitajika.

Kihenzile amemuomba Waziri Gwajima kuikumbuka Taasisi hiyo hasa pale inapotokea miradi na michango kutoka nje kutokana na kazi kubwa inayofanywa na taasisi hii kwenye kukabiliana na matukio ya dharura.

Hata hivyo, Kihenzile hakusita kuishukuru Serikali kupitia Wizara hiyo kwa kutoa fursa kwa shirika hilo katika utoaji huduma hasa kwenye maeneo ya makambini ambazo zimesaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua.

Kihenzile amesema, hii ni mara ya kwanza, kwa shirika hilo kupokea Ugeni wa Waziri wa sekta ya Afya hapa nchini toka kuanzishwa kwake na kwao hii ni ishara ya maono makubwa katika kutambua mchango wa wadau na mwelekeo mzuri wa sekta ya afya kuimarisha ushirikiano na mshikamano na wadau.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com