KAMPUNI ya Geita Gold Mine (GGML) imeibuka kuwa moja ya makampuni kinara kwa ulipaji kodi Tanzania kuelekea miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
Hayo yamebainishwa juzi Visiwani Zanzibar baada ya Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi kuitunuku cheti cha cha kutambua mchango wa GGML katika ulipaji kodi bora.
Rais Dk. Mwinyi alimkabidhi cheti hicho Makamu wa Rais wa GGML anayesimamia miradi endelevu, Simon Shayo hii ikiwa ni baada ya kampuni hiyo kuibuka mshindi wa pili kwa kulipa kodi ya zaidi ya Sh bilioni 338 kwa Serikali ya Tanzania.
Rais Dk. Mwinyi alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa kongamano la maonesho ya bidhaa za viwanda ambalo pia lilikuwa maalumu katika kujadili changamoto na mafanikio ya maendeleo ya uwekezaji kwa kipindi cha miaka 60 tangu Tanzania ipate uhuru mwaka 1961.
Awali Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) Bi. Suzanne Ndomba- Doran amesema cheti ni ishara ya kutambua waajiri wanaounga mkono juhudi za serikali.
“Chama cha waajiri na ofisi ya waziri Mkuu uwekezaji, tunawapatia cheti waajiri ambao wanatoa ajira kwa wingi katika ajira za moja kwa moja lakini pia sio za moja kwa moja katika mnyororo wa thamani,” alisema.
Mbali na ulipaji wa mapato ya Serikali na uwekezaji kwenye jamii, Kampuni hiyo imetoa ajira kwa Watanzania zaidi ya 5,000 ikiwa ni pamoja na wale wanaofanya kazi chini ya wakandarasi wa kampuni hiyo.
Aidha, hadi kufikia mwaka huu takriban asilimia 98 ya wafanyakazi wa GGML na asilimia 82 ya menejimenti ni Watanzania.
Malengo ya kampuni hiyo ni kuendelea kuwa mdau mwaminifu wa maendeleo kwa Tanzania ikiwa ni pamoja na kuwa sehemu ya mustakabali wa kujenga uchumi wa viwanda na kufikia dira ya 2025 ambapo sekta ya madini imelengwa kuchangia walao 10% ya pato ghafi la taifa.
Kwa kipindi cha miaka minne mfululizo GGML imekuwa mdau mkubwa wa maendeleo kwani kwa kushirikiana na Serikali mkoani Geita imetekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kupitia fedha za wajibu wa Kampuni kwa Jamii (CSR) zenye gharama zaidi ya Shilingi bilioni 36.
Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi (kushoto) akimtunuku cheti, Makamu wa Rais kampuni ya GGML anayeshughulikia miradi endelevu, Simona Shayo (kushoto). Cheti hicho kilichotolewa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) na Ofisi ya Waziri Mkuu kinalenga kutambua mchango wa GGML katika uajiri na ulipaji kodi bora kwa Serikali ya Tanzania.
Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi (kushoto) akimtunuku cheti, Makamu wa Rais kampuni ya GGML anayeshughulikia miradi endelevu, Simona Shayo (kushoto). Cheti hicho kilichotolewa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) na Ofisi ya Waziri Mkuu kinalenga kutambua mchango wa GGML katika uajiri na ulipaji kodi bora kwa Serikali ya Tanzania.
Social Plugin