Wanakwaya wakicheza kabla ya kuangamia mtoni
Video ya kugusa moyo inayoonyesha namna wanakwaya wa Mwingi walisakata densi kabla ya ajali ya kutamausha iliyoangamiza maisha ya wengi wao, imevunja nyoyo za wanamtandao wengi.
Wanakwaya hao walikuwa safarini kuhudhuria hafla ya harusi wakati walikutana na mauti yao katika mto uliofurika wa Enziu mchana wa Jumamosi, Disemba 4,2021.
Walikuwa wanaelekea Nuu kwa harusi wakati walishuka kutoka kwenye basi mwendo wa saa nne 10:30 asubuhi kusubiri mawimbi ya maji kutulia ili waweze kuvuka mto huo Huku wakisubiri mawimbi hayo kutulia, walijifunza nyimbo ambazo walikuwa wanapania kuwatumbuiza wageni nazo katika harusi hiyo.
Wakiwa wamevalia nguo za manjano, wanakwaya hao wanaonyeshwa wakifurahi na kusakata densi mara ya mwisho.
Saa chache kabla ya mwendo wa saa 1:30 mchana, walimshinikiza dereva avuke mto huo uliokuwa umefurika sababu ya kuchelewa kuhudhuria harusi.
Pia waliamini itakuwa vyema kuvuka mto huo sababu magari mawili na trekta yalivuka salama. Hata hivyo, walikumbana na mauti yao baada ya basi hilo kuingia ndani ya mtaro na kuzama ndani ya mto huo mashahidi wakitazama na kushindwa cha kufanya.
Shughuli ya uopoaji bado inaendelea baada ya mkasa huo ambao umewacha taifa na majonzi huku miili 23 ikiopolewa. Rais Uhuru Kenyatta alijiunga pamoja na viongozi wengine kuomboleza pamoja na familia zilizopoteza wapendwa wao.
Katika taarifa siku ya Jumapili, Disemba 5, kiongozi wa taifa aliwatakia manusara wa ajali hiyo waliokimbizwa katika Hospitali ya Mwingi Level Four afueni ya haraka.
Rais aliwaomba Wakenya kufuata maagizo ya serikali ya kutovuka mito iliyofurika hususan kipindi hiki cha mvua.
Pia iliibuka kwamba watu 15 wa familia moja waliangamia katika ajali hiyo baadhi yao akiwa Jane Mutua ambaye ni msichana wa waliokuwa wakifanya harusi.
Social Plugin