Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Simiyu Shemsa Mohamed (kulia) akimtisha ndoo ya maji Penina Magashi mkazi wa mtaa wa Shimbale kata ya Mhango Halmashauri ya mji wa Bariadi mara baada ya kukagua ujenzi wa mradi huo wa maji.
**
Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
WAKAZI zaidi ya 3900 wameanza kunufaika na mradi wa maji ya kisima kirefu uliotekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) katika mitaa ya Isanga na Shimbale, kata ya Mhango, Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu.
Kukamilika kwa mradi huo pia kutahudumia kituo cha afya Ngulyati pamoja na wananchi ambapo kisima hicho kina uwezo wa kuzalisha lita za ujazo 5,400 kwa saa, sawa na lita 86,400 za maji kwa siku.
Hayo yalibanishwa jana na Meneja wa RUWASA wilaya ya Bariadi Mhandisi Mapengu Gendawi wakati akiwasilisha taarifa ya mradi huo kwenye kamati ya siasa ya mkoa wa Simiyu ilipotembelea kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM.
Mhandisi Gendawi alisema awali kisima hicho kilikuwa kinahudumia kituo cha afya Ngulyati pekee, kutokana na uzalishaji wa maji katika kisima hicho kuwa mkubwa kuliko mahitaji ya kituo cha afya, waliamua kukipanua ili kuwafikishia wananchi na taasisi zingine.
‘’Kupitia bajeti ya mwaka 2020/21 RUWASA ilitenga fedha kiasi cha shilingi milioni 237 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo kwa kutumia wataalamu wa ndani, ujenzi wa tanki lenye ujazo wa lita elfu 50, ujenzi wa vituo tisa vya kuchotea maji na mradi huu umekamilika kwa asilimia 95’’ alisema Mhandisi Gendawi.
Alisema kukamilika kwa mradi huo utasaidia wananchi kupata huduma ya maji safi na salama tofauti na zamani ambapo walikuwa wanategemea visima vya pampu za mkono na wataondokana na kutumia muda mwingi kutafuta maji.
Petro Nkwabi mkazi wa mtaa wa Isanga aliipongeza serikali kupitia RUWASA kwa kutekeleza mradi huo ambao umekuwa mkombozi kwao sababu huko nyuma walitumia maji ya bwawani ambayo hayakuwa safi na salama.
Naye Penina Magashi mkazi wa mtaa wa Shimbale aliishukuru serikali chini ya Rais Samia Suluhu kwa kuendelea kutekeleza miradi ya maji ambayo kwa sasa imeanza kuwanufaisha wananchi hasa kuwatua ndoo kichwani wakina mama.
‘’Tunaishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia kwa kuendelea kututua ndoo kichwani wanawake wenzake kwa kuendelea kutekeleza miradi ya maji, kwa sasa tunapata maji karibu na maeneo yetu…tunatumia muda mwingi sasa kufanya shughuli za maendeleo badala ya kutafuta maji’’ alisema Penina.
Akitoa salama za chama, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu Shemsa Mohamed aliwapongeza RUWASA kwa kuendelea kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji vijijini.
Alisema huko nyuma kulikuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji, lakini kwa sasa wakala huyo ameendelea kutekeleza miradi kwa wakati na ufanisi na wananchi wengi wameanza kunufaika na miradi ya maji.
‘’Rais Samia alisema anaenda kumtua mama ndoo kichwani, hivyo kukamilika kwa miradi hii ni utekelezaji wa Ilani na maagizo ya Rais, RUWASA tuendelee kuhakikisha eneo lenye mradi wa maji unafanyika na kufanikiwa kwa haraka ili wananchi waanze kupata maji’’ alisema Shemsa na kuongeza.
MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Simiyu Shemsa Mohamed (kulia) akimtisha ndoo ya maji Penina Magashi mkazi wa mtaa wa Shimbale kata ya Mhango Halmashauri ya mji wa Bariadi mara baada ya kukagua ujenzi wa mradi huo wa maji.
MENEJA wa RUWASA wilaya ya Bariadi Mhandisi wa Mapengu Gendawi (aliyenyoosha mkono) akitoa maelekezo kwa viongozi wa chama na Serikali namna waliyotekeleza mradi wa maji Ntuzu, katikati ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu Shemsa Mohamed.