Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JKT, DUWASA NA TFS WAPANDA MITI ENEO LA HIFADHI YENYE CHANZO CHA MAJI MZAKWE DODOMA


Mkurugenzi Ofisi ya Rais,Mazingira Dkt. Andrew Komba akipanda miti katika eneo la hifadhi ya maji Mzakwe-Dodoma.(Picha na Dotto Kwilasa)
Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano-Duwasa,Sebasti Warioba akipanda miti katika eneo la Mzakwe ikiwa ni ishara ya kuenzi mazingira.


Na Dotto KWILASA,Malunde 1 Blog, DODOMA.

OFISI ya Makamu wa Rais ( Mazingira) kwa kushirikiana na Jeshi la kujenga Taifa (JKT), Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Jijini Dodoma (DUWASA) na Wakala wa misitu Tanzania(TFS)wameendesha zoezi la upandaji miti katika eneo la hifadhi yenye chanzo cha maji Mzakwe Jijini Dodom huku wakiwataka wananchi wanaoishi karibu na eneo hilo kuzingatia kanuni za utunzaji.

Hayo yamejiri leo Jijini hapa katika eneo hilo la uhifadhi chanzo cha maji Mzakwe wakati wa zoezi la upandaji miti lililofanywa na wadau mbalimbali wa mazingira kwa lengo la urejeshaji wa miti iliyopunguzwa na kutunza mazingira.

Akiongea wakati zoezi hilo likiendelea, Mkurugenzi Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira Dkt. Andrew Komba amesema eneo hilo limekumbwa na uharibifu wa mazingira ambapo miti iliyokuwa imepandwa awali imechomwa moto na hivyo kuisababishia hasara Serikali.

Kutokana na hayo ameagiza Serikali za Vijiji,Mitaa na Vitongoji vinavyozunguka eneo la hifadhi yenye chanzo cha maji Mzakwe Jijini hapa kuchukua hatua kuisaidia serikali katika kulinda eneo hilo ili liwe endelevu kwa kuleta manufaa kwa wananchi .

Amesema kutokana na kuwepo kwa vitendo vya uharibifu wa mazingira vinavyotokana na shughuli za kibinadamu ikiwemo kuchoma moto na uwindaji haramu kwenye eneo hilo kumekuwa kukisababisha mabadiliko ya tabia nchi na ukame.

"Jamii zinazoishi eneo hili zinapaswa kutambua kuwa huu msitu ni muhimu sana,tabia ya kuchoma moto ikome,tutakuja hapa mara kwa mara kufuatilia waharibifu wa miti na ikiwa kuna mtu atabainika tutamfikisha kwenye vyombo vya Dola,"ameeleza.

Aidha ametaka kila mwananchi kupanda miti katika kuelekea msimu wa mvua ili kuweza kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwani kwa sasa nchi inakabiliwa na hali ya ukame.

Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano Mamlaka ya Majisafi na usafi wa Mazingira( DUWASA) Sebastian Warioba amesema eneo hilo ni chanzo muhimu na kinawananufaisha wananchi wengi hivyo linapaswa kupewa kipaumbele Kwa kuongeza utunzaji wa miti iliyopo ikiwa ni pamoja na kuepuka uendeshaji wa shughuli nyingine za kibinadamu katika eneo hilo.

Warioba amesema eneo hilo ni moja ya hifadhi ya mabonde ya Mto Ruvu na hivyo linatunzwa kwa
mujibu wa sheria.

"Lazima wananchi wajue hili ni eneo tengefu na haliruhusiwi kufanya shughuli za kibinadamu,upatikanaji wa maji ya uhakika unatokana na utunzaji mzuri wa mazingira,"amesema.

Naye mtunzaji wa bonde la mto Wami Dodoma
Feliciana Mpanda amesema," unapotaka kupata Maji ni lazima utunze Mazingira hasa kwa kufanya ushirikiano na Wadau wengine wa Mazingira na kutaka wananchi kutunza Mazingira,ndiyo maana tupo hapa leo,"amesisitiza.

Kwa upande wake Meneja msaidizi rasilimali misitu Kanda ya kati kutoka Wakala wa misitu Nchini TFS Patricia Manonga amesema kutokana na ukuaji wa Mji umesababisha kuwepo changamoto za uharibifu wa Mazingira na tayari wameongeza doria katika eneo hilo pamoja na kutoa Elimu kwa Jamii juu ya matumizi mbadala.


Ameeleza kuwa zoezi hilo limehusisha upandaji wa miti 1000 ikiwemo ya kivuli na matunda na kwamba Mwanzoni miti mingo ilishindwa kustahimili hali ya hewa ya eneo hilo jambo ambalo awamu hii halitatokea kwa kuwa tayari limefanyiwa kazi.

"Kabla ya kupanda miti hii tulifanya utafiti na kubaini aina
ya miti inayoweza kustahimili hali ya ukame,"amesema.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com