JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia mkazi wa Buhongwa jijini humo, Rose Joshua (27) kwa tuhuma ya wizi wa mtoto wa kiume.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ramadhan Ng’anzi amesema kuwa, tukio hilo lilitokea Desemba 19, mwaka huu, saa 4:00 usiku katika eneo la Dampo Soko la Machinga, Kata ya Buhongwa, wilayani Nyamagana.
Amesema kabla ya mtuhumiwa huyo kufanya wizi huo, alijenga ukaribu na mama wa mtoto aliyeibiwa, Stella Damas (22) ambaye ni mfanyabiashara wa eneo hilo la Dampo Soko la Machinga.
“Baada ya mazoea hayo, baadaye mtuhumiwa alimuomba mama huyo amsaidie kumbeba mtoto wakati akiendelea na shughuli zake za biashara kisha akatoweka nae kwenda kusikojulikana,” amesema.
Kamanda Ng’anzi amesema baada ya kitendo hicho, mama wa mtoto alitoa taarifa polisi ndipo ufuatiliaji wa haraka ulifanyika kwa kushirikiana na polisi Mkoa wa Kigoma na mtuhumiwa alikamatwa mkoani Kigoma na kumuokoa mtoto akiwa hai na mwenye afya njema.
“Uchunguzi wa awali umebaini mtuhumiwa alifanya uhalifu huo ili kunusuru ndoa yake baada ya kukosa mtoto kwa muda mrefu,” amesema
Social Plugin