Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MCHUNGAJI MALAGILA : IMBENI NYIMBO ZA KULETA MATUMAINI,FARAJA KWA WALIOKATA TAMAA


Na Dinna Maningo, Tarime

MUZIKI wa Dini ni muhimu katika ibada kwakuwa upo ili kumtukuza Mungu,kuwaongoa watu ili wamche Mungu na kumtumikia pamoja na kuwapa faraja na matumaini wale waliokata tamaa.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Muziki Mchungaji Winner Malagila wa Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA) Jimbo la Mara  wakati akiweka wakfu na kuiombea Dvd Vol.3 yenye jina la HABARI NJEMA TARIME CENTRAL SDA CHOIR yenye nyimbo 10,uzinduzi uliokwenda sambamba na changizo la fedha za kununua vifaa vya muziki.

Mch. Malagila alisema wapo watu nje ya kanisa wanatamani kupata injili kwa njia ya kusikiliza nyimbo za dini na wengine kusikiliza ili kuwapa faraja lakini baadhi ya nyimbo hazigusi mioyo ya watu wala kumtukuza mungu.

"Imbeni muziki ili ulete matumaini kwa watu wasio na matumaini,je muziki unaoimba utaleta faraja kwa yule asiye na faraja ?je ni muziki ambao utamfanya yule aliyekata tamaa arudi kutokata tamaa,kuna watu wanakumbana na shida mbalimbali wamekata tamaa, je nyimbo zenu zinawafariji na kuwapa matumaini ?" alihoji.

Aliongeza kuwa nyimbo uleta burudani lakini katika burudani hiyo iwe ni sehemu ya kuwaongoa watu wamjue Mungu na  kuleta mabadiliko ndani ya jamii.

"Tuimbeje wimbo wa bwana katika nchi! suala la muziki ni la muhimu sana katika ibada,ibada ililetwa kwa ajili ya kumtukuza bwana mungu,swali langu je uimbaji wetu utamwinua bwana?je albamu yako itaishia tu kuburudisha?tutunge nyimbo ambazo zitabariki watu.

" Kuna nyimbo zinaimbwa ni kero ukiimbwa mtu anazima TV au Redio maana haimgusi wala kumfanya ajifunze kitu kupitia wimbo huo,siyo dhambi kuimba nyimbo kwa kutumia ala za muziki shida iliyopo je hizo nyimbo zinazoimbwa kwa ala za muziki zinatumukaje katika kubariki watu?"alihoji Malagila.

Akisoma Taarifa ya kwaya ya Tarime Kati iliyozindua albamu ya tatu, Beatrice Kennedy afisa miradi ya kwaya katika kanisa hilo la Tarime kati,alisema kuwa  kwaya hiyo ina waimbaji 42 kati ya hao wanawake ni 29 na wanaume ni 13,wanaoimba sauti ya kwanza wapo 10,sauti ya pili 19,sauti ya tatu ni 9 na sauti ya nne ni wanne na kwamba.

Beatrice aliongeza kuwa lengo la kufanya harambee ya fedha za ununuzi wa vifaa ni kubadili uimbaji kutoka kizamani uimbaji usio wa kutumia vifaa vya muziki (anolojia)na kwenda katika uimbaji wa kisasa (kidigitali) wa kutumia vifaa vya muziki.

Alizitaja nyimbo zilizomo kwenye albamu hiyo ni Watu wa Dunia hii,Kiumbe cha thamani,Habari njema,Ibada,Mafanikio,Ndoa, Musa,Omosani,Mwanampotevu na Hubiri la Yesu.

Mwenyekiti wa kwaya hiyo Mwl. Chacha Heche aliwashukuru washiriki na wageni waalikwa kwa kutoa fedha zao ili kununua vyombo ambapo zaidi ya milioni 15 zilichangwa,ahadi fedha zaidi ya milioni 4 na vifaa mbalimbali vilivyotolewa vyenye thamani ya zaidi ya milioni moja.

"Tunawashukuru sana kwa michango, malengo yetu ya fedha za kununua vyombo vya muziki,kuanzisha online tv na  blog ya kanisa, bajeti tuliyopanga ni Milioni 30, kwaya imechangiwa fedha zaidi ya milioni 20 na wengine wataendelea kutoa,tutanunua vitu mbalimbali kama kamera kubwa,meza,kabati,viti vya maktaba na kufunga mfumo wa kwaya", alisema Chacha.

Katika uzinduzi huo mgeni rasmi alikuwa ni Josephati Chacha,kwaya zilizoshiriki ni kwaya ya Nuru- Kibara kutoka wilaya ya Bunda,Oboke kutoka Shirati wilaya ya Rorya,Itununu kutoka wilaya ya Serengeti ,Nyamorege-Sirari,Majengo na Tarime youth za kutoka wilaya ya Tarime.

Kwaya ya Tarime Kati SDA
Kwaya ya Nuru-Kibara wilayani Bunda

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com