Mkurugenzi wa Shirika la Kivulini, Yassin Ally (kushoto), Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu (kulia).
***
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mkurugenzi wa Shirika la kutetea Haki za Wanawake na Watoto KIVULINI, Yassin Ally amepongeza dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kutaka kuitenga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutoka kwenye ujumuishi huo hadi kujitegemea kuwa Wizara ya Afya ili kupambana na majanga yanayoendelea duniani na kuboresha huduma ya afya nchini.
Akizindua kamati ya ushauri ya kitaifa kuhusu utekelezaji wa ahadi za nchi kwenye jukwaa la kizazi chenye usawa leo Desemba 16,2021 jijini Dodoma, Rais Samia amebainisha kuwa Wizara ya Afya ya Tanzania bara na Visiwani inapaswa kuondolewa kwenye vipengele vya maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Rais Samia amesema sababu ya kuitenga Wizara hiyo ni kufuatia kutotimia kwa malengo mengi yanayowekwa kwenye Wizara hiyo kutokana na mlundikano wa vipengele nyingi ndani ya Wizara moja.
“Maamuzi yangu ni kuitenga Wizara itakayoshughulikia Jinsia Maendeleo ya Wanawake kutoka kwenye kuchanganywa na Wizara ya Afya kwa sababu tukiweka Wizara ya Afya na mambo mengine na hali tuliyonayo sasa hivi duniani Sekta ya Afya peke yake inachukua sura kubwa",amesema Rais Samia.
“Tukiiweka Wizara ya Afya na mambo mengine kama haya na ukiunganisha na yanayoendelea duniani tunakuwa tunaiminya. Lakini kama tutaitenga Wizara hii na mambo haya itaweza kufanya kazi vizuri,” amesema Rais Samia.
Aidha Rais Samia ameongeza kusema kuwa atazungumza suala hilo na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ally Mwinyi ili kuona namna ya kufanikisha adhima hiyo.
Kufuatia hatua hiyo, Mkurugenzi wa Shirika la kutetea Haki za Wanawake na Watoto KIVULINI, Yassin Ally amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake makubwa na uamuzi wake wenye umuhimu mkubwa na wenye tija wa kutenganisha Wizara ya Afya ,Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto akieleza kuwa ni ukweli usiopingika wizara hiyo ndio muhimili muhimu wa maendeleo na jitihada za serikali kutokomeza umaskini kuelekea Tanzania ya Viwanda na Uchumi wa Kati.
“Faida za uamuzi huu wa kutenganisha Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na watoto ni kwamba Wizara na Waziri mwenye dhamana ya maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto itapunguza mzigo mzito na pia kutaongeza bajeti na kusimamia, kuratibu na kuhakikisha Wizara na Halmashauri zote nchini zinatenga bajeti ya utekelezaji Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na watoto (MTAKUWWA 2017/2018-2021/2022 ) na Sera na Mipango yote ya Wizara”, amesema Mkurugenzi wa Shirika la KIVULINI lenye makao makuu yake mkoani Mwanza.
“Uamuzi wa Mhe. Rais Samia una faida kubwa sana ikiwemo kupunguza mzigo mkubwa na kuongeza ufanisi hususani katika kusimamia Mipango, Sera na Bajeti ikiwemo kuhakisha Wizara husika, Mikoa na halmashauri zote nchini zinatenga bajeti kutekeleza Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA), kuratibu na kushirikiana na wadau wa maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto nchini”,ameongeza Ally.
Social Plugin