Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Mwita Waitara, akizungumza na Wakuu wa Taasisi na Wafanyakazi wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, (hawapo pichani), wakati wa kikao kazi kilichofanyika leo Desemba 8,2021 jijini Dodoma.
Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS),Mhandisi Salome Kadunda akitoa taarifa ya Utekelezaji wa wakala huo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Mwita Waitara (hayupo pichani), katika kikao kazi kilichofanyika leo Desemba 8,2021 jijini Dodoma.
Baadhi ya Mameneja,Wakuu wa Taasisi na Wafanyakazi wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Mwita Waitara( hayupo pichani),wakati wa kikao kazi kilichofanyika Desemba 8,2021 jijini Dodoma.
**
Na Dotto Kwilasa, Malunde 1 blog-DODOMA.
MAMLAKA ya viwanja vya ndege nchini (TAA) imeagizwa kuongeza umakini katika ukaguzi wa viwanja vyote vya ndege ili kudhibiti mlipuko wa wimbi la nne wa ugonjwa wa COVID 19 ambao kwa sasa unatajwa kuwa na kirusi kipya cha Omicron.
Maagizo haya yanakuja baada ya hivi karibuni kuibuka taarifa zilizodai kuna abiria aliyetokea hapa nchini na kuelekea India na kukutwa na kirusi hicho kitu ambacho Serikali imekanusha.
Aidha hatua hii inakuja kipindi ambacho dunia kwa sasa imeingia kwenye wasiwasi kutokana na kuendelea kusambaa kwa kirusi hicho ambacho tayari mataifa kadhaa duniani,raia wake wamezuiliwa kuingia kwenye baadhi ya mataifa ya Ulaya na Amerika.
Wakati hali ikiwa hivyo ndipo Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mwita Waitara akizungumza na watendaji wa wizara hiyo jijini Dodoma akataka TAA kuzidisha zaidi umakini kwenye ukaguzi ili kudhibiti wale na kuwabaini wenye kirusi cha Omicron na kwamba ikitokea ni kweli wapo basi iwe rahisi kuwekwa kizuizini kuwalinda wengine.
"Hakikisheni mnaimarisha ukaguzi, na watu wote lazima wakaguliwe bila kujali aina ya hati za kusafiria maana suala la usalama wa nchi halina dhamana ya nani ni nani,mbona sisi tukiwa Nchi za nje hata kama una kibali cha kidiplomasia lakini bado tunakaguliwa,"amesema Waitara.
Mbali na hayo utata kwenye vizibiti mwendo kwenye magari nao ukaonekana kumkera naibu Waziri huyo ambapo akiwa hapo pia ametoa maelekezo kwa shirika la reli nchini kuitangaza tarehe maalumu ya kufanya majaribio ya treni ya kisasa na kuondoa mkanganyiko .
Sambamba na hayo ,Waitara ametumia nafasi hiyo pia kutoa maelekezo kwa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA),kuimarisha shughuli zao na kuboresha utendaji wao ili kuendana na soko.
Amesema utendaji wa TEMESA umekuwa hauna tija kutokana na sababu aliyoitaja kuwa hauridhishi na kusababisha kukosa soko la magari ya serikali na ya viongozi.
Kutokana na hali hiyo, amewataka kuanzia mwezi Januria mwakani waimarishe utendaji wao na kwamba wakienda kinyume na maagizo hayo sheria Serikali haitawavumilia.
"Ninapowakosoa sio kwamba nawaonea ,nadhani hata ninyi wenyewe mnajua hamko vizuri kiutendaji,kuna wakati mtu unawaza hata umuhimu wenu hauonekani, nadhani mnapaswa kujielewa na mtimize vizuri majukumu yenu,"amesema .
Pamoja na hayo amewaelekeza Mamlaka ya huduma za Usafiri Ardhini(LATRA), kuhakikisha inashughulikia malalamiko ya wadau ikiwemo Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania(TABOA).
”Kumekuwa na malalamiko kutoka kwa chama cha usafirishaji
nchini TABOA kutokana na mzabuni huyo kushindwa kudhibiti mwendo mpaka apige simu makao makuu ili kujua dereva anakwenda mwendo gani,hivi vitu jamani havivumiliki kabisa,"amesema Naibu Waziri huyo.