ADA MPYA ZA UZOAJI TAKA MJINI SHINYANGA ZAZUA GUMZO... MKURUGENZI WA MANISPAA KUTOA UFAFANUZI KESHO


Zoezi la uzoaji wa taka ngumu likiendelea katika ghuba la Soko Kuu Mjini Shinyanga leo Novemba 2,2021
Nyaraka ya Jedwali la ada za uzoaji wa taka ngumu kwa mujibu wa sheria ndogo za Manispaa ya Shinyanga linalosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Wakazi wa Manispaa ya Shinyanga wamepatwa na mshangao baada ya Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kupandisha ghafla ada za uzoaji wa taka ngumu kwa mujibu wa sheria ndogo za Manispaa ya Shinyanga hali ambayo imezua mijadala mbalimbali mtaani na kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuanza kutumika Desemba 1,2021.

Katika malalamiko hayo mfano wamesema mtu aliyekuwa analipa shilingi 2,000/= sasa atalipia shilingi 5000/= na upande wa taasisi zilizokuwa zinalipa shilingi 3000/= sasa watalipa shilingi 10,000/= huku aliyekuwa analipia shilingi 10,000/= sasa atatakiwa kulipa shilingi 50,000/= kwa mwezi.

Kupitia majukwa mbalimbali ya mitandao ya kijamii wakazi wa Manispaa ya Shinyanga wanasema licha ya kwamba jambo la ada za taka ni la lazima lakini ada hizi mpya ni kubwa kuliko gharama za awali hivyo kuiomba serikali kuangalia namna ya kupunguza ada hizo huku wakiomba ulipaji wa ada ya taka uendane na thamani ya fedha na kusisitiza wakusanya taka kukusanya taka kwa wakati kwani wamekuwa wakichelewa kuchukua taka.


Wamesema hali ya zoezi la ukusanyaji wa taka katika Manispaa ya Shinyanga limekuwa halina tija kwa kuwa wananchi wenyewe wamekuwa wakitumia vifaa vyao na gharama zao kuondoa taka kutoka kwa watu wengine wa mitaani na kubainisha kuwa wahusika wa Manispaa wa kuondoa taka kutofikia mitaa yao.


“Hii tozo ya taka inatisha mfano Hotel jana tumeambiwa kutoka 10,000/= mpaka 50000. hii ni asilimia ngapi imeongezwa? kweli inashangaza sana , lakini pia hawa wakusanya taka hawakusanyi taka kwa wakati mara nyingi hadi tunatafuta watu binafsi wenye matolori tunalipa wenyewe maana taka zinajaa na hawaijii ,hili ongezeko la tozo za taka linaumiza wananchi”, wamesema wananchi.


“Utaratibu wa kutaka kupandisha hata sent moja kwenye halmashauri zetu nijuavyo hatua zinazotakiwa ni vikao vya wadau husika , vikao vya Madiwani na Waziri husika kisha wanatuletea wananchi, sasa hatuoni hatua ya 1 na 3. Ipo hivi, hata bunge linapitisha sheria na haiwezi kutumika mpaka Mhe. Rais atie mkono kwa kua- ascend”,wamesema.


“Je mnaweza kutuletea pia wapi Waziri mwenye dhamana alikubali sheria hii ndogo itumike!?, Unaweza tuwekea mihtasri ya vikao vya wananzengo kukubali kupanda kwa ada/ ushuru huu!? Kama hakuna hivyo viwili, jamaa watakuwa wamepandisha isivyotakiwa”, wamesema.


Hata hivyo Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Mhe. Jomaary Mrisho Satura alipotafutwa kwa njia ya simu na waandishi wa habari amesema kesho Ijumaa Desemba 3,2021 atakutana na waandishi wa habari kwa ajili ya kutolea ufafanuzi suala hilo la ada za uzoaji wa taka ngumu .

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post