TISHA NA TEMBOCARDVISA YAFANIKISHA MIAMALA YA MABILIONI

Mwandishi Wetu.
Mwezi mmoja tangu izinduliwe kampeni ya “Tisha na TemboCardVisa” katika mikoa ya kanda ya kaskazini inayolenga kuhamasisha miamala ya kidijitali, mwitikio wa wateja umefanikisha miamala ya mabilioni mpaka sasa.

Kwa kushirikiana na kampuni ya Visa International, Benki ya CRDB ilizindua kampeni hiyo Desemba mosi 2021 ukiwa ni utekelezaji wa mkakati wa kujenga utamaduni wa kufanya miamala ya kidijitali huku wateja wanaoshiriki hilo wakijiweka kwenye nafasi ya kushinda zawadi mbalimbali ikiwamo kwenda kushuhudia kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) litakalofanyika nchini Cameroon mwaka 2022.

Tangu kuzinduliwa kwa kampeni hiyo katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro kulikojumuisha matangazo ya barabarani, uwezeshaji wa vituo vya huduma zikiwamo baa, Migahawa, vyuo vikuu, maduka ya rejareja na supermarkets na michezo hasa riadha, pamoja na ziara kwenye vyombo vya habari, Jumla ya miamala 136 yenye thamani ya Sh17 bilioni imefanyika.

Kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata taarifa za kampeni hii, maofisa wa Benki ya CRDB walitembelea vyombo vya habari wakianza na kituo cha Sunrise FM cha jijini Arusha. Maofisa hao walienda katika kituo hicho Desemba 10 mwaka 2021 na kutoa elimu kwa wananchi.
Licha ya kuzungumza na wananchi wa kituo hicho cha redio, huduma ya kulipa kwa kadi ilizinduliwa Pillars ambako maofisa wa benki walizungumza na wateja.
“Licha ya kuzungumza na wateja, tulitoa zawadi kuonyesha shukrani kwao kwa kuendelea kutumia huduma zetu,” anasema Erica Mwaipopo, meneja mwandamizi wa biashara ya kadi Benki ya CRDB.

Maeneo mengine ambako huduma ilizinduliwa ni katika vituo vya mafuta kikiwamo cha Great North.

Wateja wanaoenda katika maeneo mbalimbali kufanya manunuzi ikiwamo TFA Mall nao wanaweza kuitumia huduma yetu kwani inapatikana hapo. Wanafunzi na wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (Muco zamani Muccobs) mkoani Kilimanjaro nao wameunganishwa ambapo kunakipengele kinacho jitegemea kwenye promosheni hii mahsusi kwa wanafunzi. Mjini Moshi, huduma hii ya kulipa kwa kutumia kadi ya TemboCardVisa inapatikana katika kituo cha Mafuta cha Oryx, Kilimanjaro Star Supermarket pamoja na baa za Kwetu Pazuri na Redstone.

Desemba 24, Erica Mwaipopo alitoa elimu kwa wananchi wa Kilimanjaro wanaosikiliza Redio ya Kili FM na wateja waliokuwepo Kwetu Pazuri, Hugo’s Garden, Kilimanjaro Star Supermarket, Redstone na Kili Home Recreation Centre walianza kunufaika na huduma hii salama na ya uhakika baada ya kuzinduliwa katika vituo hivyo huku magari ya matangazo yakizunguka mitaani kuwahamasisha na kuwawezesha wananchi kuitumia.
Wiki tatu za kujumuika na wateja, wadau na wananchi wa kanda ya kaskazini zilihitimishwa Desemba 26 ambapo elimu ilitolewa kuhusu promosheni hiyo kwa washiriki wa Siha Marathon zilizodhaminiwa na Benki ya CRDB na kampeni ya Tisha na TembocardVisa ikaongeza uhai na kunogesha mashindano hayo.

Akihimiza umuhimu wa kufanya miamala kidijitali, Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na wa Kati wa Benki ya CRDB, Boma Raballa alisema matumizi ya Huduma za Tehama yanatokana na mabadiliko ya teknolojia yanayoshuhudiwa duniani kote hivyo kurahisisha biashara hata katika kipindi cha changamoto kama janga la Uviko-19.

Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa kampeni hiyo iliyofanyika makao makuu ya CRDB jijini Dar es Salaam, Raballa alisema wateja watakaotumia zaidi kadi zao watajiweka kwenye nafasi ya kujishindia zawadi katika kipindi chote cha kampeni itakayohitimishwa Machi 2022.

“Lengo letu ni kuona Watanzania wanajenga utamaduni wa kutumia kadi zao kufanya malipo ya huduma au bidhaa wanazonunua na kuachana na utaratibu wa kutumia pesa taslimu. Katika kipindi chote cha kampeni tutatoa zawadi kwa zaidi ya washindi 80, kila mwezi tutakuwa na washindi 20,” alisema Raballa.

Kati ya zawadi ambazo wateja wanaendelea kujizolea ni kurudishiwa asilimia tano ya kiasi walichotumia, kulipiwa bili ya ununuzi walioufanya, simu janja, tablet, televisheni, seti ya sofa, home theatre, na safari ya kitalii kwenda Zanzibar au Serengeti.

Lakini, zawadi kubwa zaidi, ni safari ya kwenda Cameroon kushuhudia michuano ya AFCON. Wateja wanne watakaofanya miamala mingi zaidi kati ya Desemba 2021 na Januari 2022 wataenda Cameroon, wakipenda wanaweza kuambatana na wenza au rafiki zao, aliongeza Raballa.

Kwa wapenzi wa michezo hasa mpira wa miguu, hakuna muujiza wa kuishuhudia michuano hiyo chini ya udhamini wa Benki ya CRDB zaidi ya kushiriki kampeni hiyo kwa kutumia kadi ya TembcardVisa kufanya malipo na kuuendeleza na kujenga utamaduni huo wa kufanya miamala pasipo kutumia fedha taslimu.

Kwa wasio na akaunti ya Benki ya CRDB, wanashauriwa kufungua ili waweze kuunganishwa na TembocardVisa na kuanza kufurahia huduma hii makini huku wakijiwekea nafasi ya kujishindia zawadi zinazoendelea kutolewa na Benki hiyo. “Tumerahisisha ufunguaji wa akaunti, Kama una simu janja, pakua program ya SimBanking na ufuate hatua za kufungua akaunti ukitumia namba ya kitambulisho cha Taifa kisha omba Tembocard. Kwa wasio na simu janja wanaweza kwenda kwa wakala wa CRDB wakiwa na kitambulisho cha Taifa ili waweze kufunguliwa akaunti na kupata TemboCardVisa,” alisema Raballa.

Jinsi ya kushiriki

Ili kuwa miongoni mwa washindi, Erica Mwaipopo anasema mteja anatakiwa kutumia kadi yake ya TemboCardVisa kulipia bidhaa au huduma anazopata dukani, supermarket, mgahawani/hotelini au hata kwenye vituo vya mafuta, baa na anapofanya malipo mtandaoni ikiwamo kulipia tiketi za ndege au kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi.

Kampeni ya “Tisha na TemboCardVisa” inaenda sambamba na uzinduzi wa muonekano mpya wa kadi za CRDB TemboCard zilizoboreshwa zaidi ili kuwapa wateja uzoefu bora zaidi pindi wazitumiapo.

Kuhusu mwonekano huo mpya, Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa Benki ya CRDB, Joseline Kamuhanda anasema zimetengenezwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa inayowawezesha wateja kuzitumia kwa urahisi mahali popote.

CRDB ilikuwa Benki ya kwanza kuanzisha matumizi ya kadi za kutolea fedha nchini ilipozindua TemboCard mwaka 2002. Mpaka sasa imetoa zaidi ya TemboCard milioni tatu huku ikiungana na mifumo ya malipo ya kimataifa ya Visa, MasterCard na Union Pay.

Licha ya kulipa kirahisi kwenye maelfu ya vituo vilivyopo nchini, mteja wa Benki ya CRDB iliyoanzishwa mwaka 1996 wanaweza kuzitumia kadi zao kwenye mashine zaidi ya 460 za kutolea fedha nchini (ATM) na mashine 15 za kuweka hela.

Benki hiyo yenye matawi 198 nchini kote pamoja na matawi 12 yanayotembea, inawaruhusu wateja wake kulipia bidhaa au huduma kwenye takriban vituo 990 vilivyopo na kupata huduma kutoka kwa zaidi ya 1,769 mawakala.

Nje ya mipaka, wateja wa Benki ya CRDB wanaweza kuhudumiwa nchini Burundi ambako ina kampuni tanzu huku ikikamilisha utaratibu wa kuanza kutoa huduma nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Vilevile, wateja wanaweza kununua bidhaa mtandaoni kutoka mahali popote duniani walikojiridhisha na ubora wa bidhaa husika kasha kulipa kwa kutumia kadi ya Benki ya CRDB.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post