ALIYEFARIKI MIAKA MINNE ILIYOPITA AKUTWA HAI , AMEKATWA ULIMI


Picha haihusiani na habari hapa chini
***
- Alifariki 2017 katika Hospitali ya Wilaya Geita
-Akutwa amekatwa ulimi hawezi kuongea


NA BALTAZAR MASHAKA, Geita
JESHI la Polisi Mkoa wa Geita linachunguza tukio la Mtoto Leonard Morisha (11), mkazi wa Kijiji cha Ngemo, Wilaya ya Mbogwe,anayedaiwa kufariki dunia miaka minne iliyopita kisha kupatikana hai wilayani Kahama.


Mtoto huyo aliyefariki Juni 27, 2017 katika Hospitali ya Wilaya ya Geita kwa ugonjwa wa upungufu wa damu (Anemia) na kuzikwa kijijini kwao, anadaiwa kupatikana Oktoba mwaka huu akiwa hai katika Kijiji cha Segese,Msalala wilayani Kahama.


Akizungumza kwa simu , Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Henry Mwaibambe, amesema mtoto huyo alipatikana Oktoba 2021,usiku katika Kijiji cha Segese,Wilaya ya Kahama akirandaranda madukani lakini akiwa hana uwezo wa kuongea kutokana na kukatwa ulimi.


Alisema mtoto huyo alichukuliwa na mlinzi wa maduka hayo, Emmanuel Kusiga na kwenda naye nyumbani kwake kisha kutoa taarifa kwa uongozi kwa serikali ya kijiji hicho na ikatagaza shuleni,sokoni na kwenye nyumba za ibada ili kuwapata wazazi wake.


Mwaibambe alisema Disemba 12,mwaka huu, wakazi wa Kijiji cha Ngemo wanaofanya vibarua vya kulima mashamba kwenye Kijiji cha Segese,walimwona na kumtambua mtoto huyo wakatoa taarifa kwa mama yake mzazi.


Alieleza kuwa jeshi hilo kwa pamoja na mama huyo, Thereza Lusolela (48) walikwenda alikokuwa Leonard ambapo mtoto huyo alimtambua mama yake na kumkimbilia huku akiangua kilio ambapo mwanamke huyo alikiri kumtambua kuwa ni mwanaye aliyefariki miaka 4 iliyopita.


“Kabla Thereza alimtambua Leonard kuwa ni mwanaye kwa kutaja alama alizonazo mwilini ambazo ni kovu la jeraha kwenye goti la mguu wa kulia na kiafuani akidai aliunguzwa kwa moto wa sigara na baba yake,”alisema Mwaibambe.


Alieleza zaidi baada ya kutambuliwa walimpeleka Leonard katika Kituo cha Afya Masumbwe kwa uchunguzi wa afya yake akaonekana kuwa na afya njema, isipokuwa hawezi kuongea kutokana na kukatwa sehemu kubwa chini ya ulimi.


“Ajabu mtoto huyo alipomwona mama yake alimtambua alilia sana na akamkimbilia, pia alipatambua nyumbani kwao pamoja na marafiki zake aliokuwa akicheza nao,”alisema Mwaibambe.


Kamanda huyo wa polisi aliongeza kuwa,waliomba kibali cha mahakama kwa mujibu wa sheria ili kufukua kaburi alimozikwa mtoto huyo na baada ya kukipata lilifukuliwa mbele ya wananchi akiwemo mama mzazi wa mtoto huyo.


“Disemba 16, mwaka huu, majira ya saa 4:00 asubuhi kabla ya kufukua kaburi hilo,Thereza (mama wa mtoto)alieleza jinsi mwanaye alivyozikwa kuwa alivishwa bukta na shati,akazungushiwa vitenge viwili na kuwekwa ndani ya jeneza,”


“Kaburi lilipofukuliwa ajabu hatukukuta nguo (vitenge), jeneza wala ubao,bali nguo (bukta na shati) zikiwa hazijachakaa ambazo mama huyo alizitambua,pia tulikuta suruali ya mtu mzima iliyotambuliwa kuwa ya baba yake, marehemu Morisha John, aliyefariki mwaka 2019 kwa kidonda baada ya kuunguzwa na pikipiki pamoja na mifupa,”alifafanua Mwaimbambe.


Alieleza zaidi kuwa walichukua sampuli kwa uchunguzi wa kisayansi utakaotoa majibu ya kitaalamu lakini kwa jicho la kawaida la kibinadamu, mtoto ni huyo huyo.


Aidha kwa mujibu wa kamanda huyo wa polisi wameshaurina na Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe,Mhandisi Charles Kabeho,mtoto huyo arudi kwenye mfumo wa elimu aendelee na masomo na kuomba tatizo na kutoongea baada ya kukatwa ulimi kwa chini, hospitali kubwa za Muhimbili, Bugando na KCMC waone namna ya kumsaidia aweze kuongea.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post