Na Dotto Kwilasa Malunde 1 blog,DODOMA.
JESHI la Polisi Mkoani Dodoma linawashikilia wahamiaji haramu 51 ambao ni raia wa Ethiopia kwa tuhuma za kuingia nchini bila kibali.
Wahamiaji hao walikuwa wakielekea Mikoa ya Kusini mwa Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dodoma Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma Kamishina msaidizi mwandamizi wa Polisi SACP,Onesmo Lyanga amesema tukio hilo limetokea Disemba 27 Mwaka huu katika eneo la kizuizi cha Bereko Wilayani Kondoa Mkoani Dodoma.
"Tunawashikilia tunaendelea na taratibu za kisheria na wasafirishaji wa wahamiaji haramu wawili ambao ni Watanzania nao tunawashikilia,"amesema.
Amesema watu hao wamekamatwa wakiwa kwenye gari aina ya fuso lenye namba za usajili T592AUE lililotumika kuwabeba wahamiaji hao.
Aidha Kamanda Lyanga ametoa onyo kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri kutotumika kusafirisha wahamiaji haramu,madawa ya kulevya au nyara za Serikali na kuwataka watanzania kuwa wazalendo.
Kwa upande wake Mrakibu mwandamizi wa uhamiaji Adam Mkuyu ambaye ni Kaimu Afisa uhamiaji Mkoa wa Dodoma amewashukuru wananchi kwa kutoa taarifa ya kulinda nchi na kuwataka kuendelea kutoa taarifa .
Aidha ametoa wito kwa wananchi ambao wanajihusisha na biashara haramu ya wahamiaji haramu kuacha mara moja bali wafanye kazi nyingine na wahamiaji haramu kufuata taratibu za nchi.
"Tunahitaji wageni hapa nchini lakini waje kwa utaratibu,mgeni yeyote anayeingia nchini anapaswa kufuata taratibu zote,"amesema.
Social Plugin