SAILI Juma (27) mkazi wa Mbeya ambaye mapema wiki hii alilala kitandani nyumbani kwao Mbeya na ghafla akaamkia juu ya mti Masasi mkoani Mtwara akiwa amelala fofo, amesafirishwa kurejea Mbeya.
Juma amerejea nyumbani kwao baada ya kuchangiwa nauli na wananchi wa Mbeya waishio Masasi. Wakizungumza na Nipashe jana, baadhi ya wananchi hao walisema wameamua kumsafirisha baada ya kuguswa na aina ya tukio lililomtokea.
Kesi Mwandisile, mwenyeji wa Mbeya anayeishi mjini hapa, alisema juzi walipata taarifa hizo kwa mtu mmoja mwenyeji wa mkoani kwao kuwa amekutwa amelala juu ya mti akitokea huko bila kujitambua.
Alisema tayari wameshamsafirisha kijana huyo baada ya kupata fedha ambazo wamechangishana ili kumwezesha kurejea Mbeya kwa ndugu zake. Licha ya kuchangishana fedha za kumsafirisha, pia alisema alipewa huduma mbalimbali zikiwamo malazi na chakula.
Mwananchi mwingine wa Mbeya, Faustine Mwakipesile, anayeishi wilayani Masasi, alisema kijana huyo amesafiri na basi la kampuni ya Sajda linalofanya safari kutoka Masasi kwenda Mbeya.
Alisema wamestaajabishwa na tukio hilo na kwamba si la kawaida kwa kuwa limevuta hisia kubwa kwa jamii na kuacha maswali mengi.
Ofisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Mji Masasi, Leila Kasunguru, alisema ofisi yake imekuwa pamoja na kijana kwa siku mbili huku akipatiwa huduma za msingi kikiwamo chakula.
Alisema ofisi hiyo ilipokea michango iliyofikia Sh. 70,000 kutoka kwa watu mbalimbali wakiwamo wa Mbeya wanaoishi Masasi. Kasunguru alisema katika fedha hizo, Sh 40, 000 amelipiwa nauli kutoka Masasi hadi Mbeya na Sh.30,000 amekabidhiwa ili kumsaidia akiwa safarini.
Juma alisema baada ya kupata fahamu anaendelea vizuri na hakuna kinachomsumbua na kwamba anawashukuru wote waliomsaidia.
“Nawashukuru wote walionisaidia kunishusha juu ya mti na kunipeleka hospitalini na wale walionichangia fedha zinazonifanya leo (jana) nianze safari ya kurudi nyumbani Mbeya,” alisema Juma.
Alisema bado hajapata ufahamu hadi sasa nini kilitokea na amewezaje kutoka Mbeya hadi kufika Masasi na kueleza kuwa yote atakwenda kuyajua atakapofika Mbeya.
Chanzo - NIPASHE
Social Plugin