Mkazi wa Kijiji cha Genkuru, tarafa ya Ingwe, Tarime mkoani Mara, Buriani Chacha, amehukumiwa kunyongwa hadi kufa
baada ya kupatikana na hatia ya mauaji.
Chacha (32) amehukumiwa baada ya kubainika kumuua Mugosi Nyagana (73) kwa kumpiga na jiwe kichwani sehemu za kisogoni akimtuhumu kuwa ni mchawi kisha kwenda kutupa mwili wake kichakani jirani na nyumba yake.
Mshtakiwa alisomewa hukumu hiyo juzi mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, John Kahyoza, katika kikao cha Mahakama hiyo kilichoketi na kuendelea na kesi wilayani Tarime.
Jaji Kahyoza alisema ushahidi uliotolewa katika kesi hiyo ya mauaji, umethibitisha bila kuacha shaka kuwa mtuhumiwa alikuwa na nia ovu ya kufanya mauaji.
“Kama ulivyoshtakiwa, mahakama hii inakuhukumu kunyong'wa hadi kufa ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye nia ya kuwadhuru wenzao na kupoteza nguvu kazi kwa familia iliyoathirika na taifa kwa ujumla," alisema Jaji Kahyoza.
Awali, Mwanasheria wa Serikali, Yese Temba, alidai mahakamani hapo kuwa mtuhumiwa alifanya mauaji hayo Aprili 18, 2018 saa 12:00 jioni katika Kijiji cha Genkuru kwa kumpiga kwa kutumia jiwe kichwani sehemu za kisogoni Mugosi Nyagana.
Temba alidai kuwa kitendo hicho kilisababisha kutokwa damu nyingi na kuharibu mfumo wa ubongo na kusababisha kifo chake.
Baada ya kufanya kitendo hicho, alidai kuwa aliuchukua mwili wa marehemu na kwenda kuutupa vichakani na kukutwa na wananchi na familia ya marehemu.
"Chanzo cha mauaji hayo ya kujichukulia sheria mkononi ni kutokana na mshitakiwa kumtuhumu Nyagana kuwa ni mchawi anaroga familia yake na mashamba yake.
Katika kesi hiyo, upande wa mashitaka ulipeleka mahakamani mashahidi wanne walioshuhudia tukio hilo wakiwamo wajukuu wa shangazi wa Nyagana na fomu namba tatu (PF3) uchunguzi wa daktari.
Kabla ya kutolewa hukumu, mshtakiwa alipewa nafasi ya kujitetea na kudai kuwa walikuwa na mgogoro wa mahari ya ndugu yao aliyeolewa na ndoa kuvurugika hivyo kutaka mahari irejeshwe hali iliyosababisha chuki na yeye mtuhumiwa kuchomewa mji wake na kuhamia Nyamongo, hivyo kuiomba mahakama imsamehe.