ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu la Katoliki la Arusha, Mhashamu Isack Amani ameonya wanafunzi wa vyuo vikuu nchini kuacha mara moja tabia ya kuishi kinyumba na wanafunzi wenzao kwani kwa kufanya hivyo wanakiuka maadili ya Mtanzania na ya dini.
Askofu Amani alisema hayo wakati akihubiri Ibada ya Mkesha wa Krismasi, iliyofanyika katika Parokia ya Uaskofuni ya Toleo la Bwana, Jijini Arusha.
Alisema baadhi ya wanafunzi wa kike wa vyuo, wamekuwa na tabia mbaya na sio nzuri kwa jamii ya kuishi kinyumba na wanafunzi wenzao wa kiume, kinyume cha maadili ya dini na sheria ya ndoa.
Askofu huyo alibainisha kuwa kwa muda mrefu wanafunzi hao wamekuwa wakistarehe na wakati mwingine kutoa mimba wanazopata wakati wakijua wazi kufanya hivyo ni kosa kisheria na kidini, hivyo jamii inapaswa kukemea hilo kwa faida ya nchi.
“Maisha hayo ya unyumba ya miaka mitatu hadi minne yamekuwa yakichukuliwa kama ya kawaida, wanaishi chumba kimoja na kitanda kimoja na wakishamaliza mahafali wanaachana… Tabia hiyo sio nzuri. Ndoa ni taasisi ambayo Mungu ameiweka kwa makusudi, ni ya usalama wa maisha ya wawili na taratibu za kuishi kwa mkataba na maagano yanayochagizwa na sheria na taratibu za dini,” alisema.
Alisema maisha ya kuishi kama mume na mke na kutoa mimba kwa wanawake baadaye huweza kuwasumbua kupata ujauzito muda wa kuoelewa kisheria unapofika kutokana na uwezekano wa kudhuru vizazi vyao.
Alisema siku ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo ni mfano wa kuigwa na wanajamii wote ambao mwisho wa siku wataishi kwenye ndoa na kuwataka kutengeneza familia zinazofanana na Familia ya Yesu, Maria na Yoseph.
Vilevile Askofu Amani alisema familia ambazo zimekosa maadili na kuwa na ukatili kwa watoto zimekuwa chanzo kwa ongezeko la watoto mitaani.
Aliwataka wanandoa kuwalea watoto malezi bora kwa njia za upole na upendo na kuacha kuzaa watoto nje ya ndoa ambao wanashindwa kuwaingiza kwenye familia, hali ambayo inachangia kuongezeka watoto mitaani.
Social Plugin