Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BALOZI LUVANDA AWASILISHA HATI ZA UTAMBULISHO KWA MFALME JAPAN

 

Balozi wa Tanzania nchini Japan Mhe. Baraka Haran Luvanda amewasilisha Hati za Utambulisho kwa Mtukufu Mfalme Naruhito wa Japan leo tarehe 27 Disemba, 2021 katika Kasri la Mfalme huyo jijini Tokyo.

Mara baada ya Mtukufu Mfalme Naruhito kupokea hati za utambulisho kutoka kwa Balozi Luvanda, amempongeza kwa kuteuliwa katika nafasi hiyo na kumtakia majukumu mema katika kusimamia mahusiano mazuri yaliyojengeka kwa miaka mingi kati ya Japan na Tanzania.

Vilevile, Mfalme Naruhito alimshukuru Balozi Luvanda kwa kumfikishia salamu kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Kadhalika, Mfalme Naruhito alimtaka Balozi Luvanda kutembelea maeneo mbalimbali ya Japan kwa lengo la kutafuta fursa za ushirikiano wa kimaendeleo, hususan pale janga la UVIKO-19 litakapokuwa limedhibitiwa.

Balozi Luvanda kabla ya kuwasilisha Hati za Utambulisho kwa Mfalme Naruhito alipata fursa ya kuzungumza na Waziri wa Fedha wa Japan Mhe. Suzuki Shunichi, ambapo pamoja na mambo mengine Balozi Luvanda, ameishukuru Japan kwa misaada na mikopo yenye masharti nafuu ya kimaendeleo inayotolewa kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, Waziri Shunichi amemhakikishia Balozi Luvanda kuwa Serikali ya Japan itaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha inafikia dira yake ya maendeleo kwa ajili ya Watanzania na kwamba Japan inaiona Tanzania kuwa mbia muhimu na wa karibu wa Japan katika medani ya kimataifa.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com