Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BENKI YA CRDB YAIBUKA MSHINDI WA JUMLA TUZO ZA NBAA




Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo akipokea tuzo ya mshindi wa jumla kwa uwasilishaji bora wa Taarifa za Fedha Nchini kwa viwango vya kimataifa, kutoka kwa Mhasibu Mkuu wa Serikali, Leonard Mkude (kushoto), katika hafla ya utoaji tuzo kwa washindi wa Shindano la Uandaaji Bora wa Hesabu kwa Viwango vya Kimataifa kwa mwaka 2020. Shindano hilo liliandaliwa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) na lilifanyika katika Kituo cha Mikutano cha NBAA Bunju Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki iliyopita. Kulia ni Mtaalamu wa Uendeshaji wa Fedha wa Benki ya CRDB, Neema Maganja.
Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo (wa saba kushoto) akiwa pamoja na wafanyakazi wa Idara ya Fedha wa Benki ya CRDB wakiwa wa tuzo ya mshindi wa jumla kwa uwasilishaji bora wa Taarifa za Fedha nchini kwa viwango vya kimataifa, waliyoipata katika Shindano la Uandaaji Bora wa Hesabu kwa Viwango vya Kimataifa kwa mwaka 2020 lililoandaliwa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) na kulifanyika katika Kituo cha Mikutano cha NBAA Bunju Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki iliyopita.
Wafanyakazi wa Benki ya CRDB Idara ya Fedha wakifurahia tuzo zao walizopata katika Shindano la Uandaaji Bora wa Hesabu kwa Viwango vya Kimataifa kwa mwaka 2020 ambapo Benki ya CRDB iliibuka kinara, lililoandaliwa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) na kulifanyika katika Kituo cha Mikutano cha NBAA Bunju Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki iliyopita.
BENKI ya CRDB imeibuka kinara katika tuzo zinazotolewa na Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA) kama taasisi ya fedha iliyoongoza kwa kuwasilisha Taarifa ya Fedha bora kwa mwaka 2020 kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.


Akizungumza wakati kukabidhi tuzo hiyo, Mhasibu Mkuu wa Serikali, Leonard Mkude aliipongeza Benki ya CRDB kwa kuendelea kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa katika utayarishaji wa taarifa zake za kifedha.

Mkude alisema kuandaa ripoti za mwaka za Mashirika na Taasisi za Umma kwa viwango vya kimataifa kunawapatia wananchi fursa ya kupima ufanisi wa utendaji kazi wa taasisi husika, kuona namna gani yanawajibika ipasavyo katika kutumia rasilimali.

“Hongereni sana Benki ya CRDB kwa kuibuka kinara wa jumla na kwa upande wa taasisi za fedha, hii inadhihirisha ni jinsi gani Benki hii imewekeza katika mifumo ya kisasa ya kutoa huduma kwa wateja lakini pia na kuwezesha kupata taarifa za kiwango,” alisema Mhe.Mkude.

Kwa upande wake Afisa Mkuu wa Fedha Benki ya CRDB, Fredrick Nsekanabo, alisema kuwa Benki ya CRDB inatambua umuhimu wa kuandaa taarifa za fedha kupitia mifumo inayozingatia viwango vya kitaifa na kimataifa. Alisema kitendo cha kupata tuzo hizo kunaifanya benki hiyo kuendelea kuongeza jitihada ili kubaki katika nafasi hiyo.

“Tumefanya uwekezaji mkubwa katika mifumo ya kidijitali hii ni pamoja na kuboresha mifumo yetu ya kukusanya na kuandaa taarifa. Tumeweza pia kuunganisha mfumo wetu wa utoaji taarifa za fedha na mfumo wa kimataifa wa kuandaa taarifa za fedha (IFRS), hii pia imechangia Benki yetu kuwa bora zaidi,” alisema Nshekanabo.

Nshekanabo alibainisha kuwa ushindi huo pia unatokana na Benki hiyo kuwa na mfumo bora wa uongozi unaozingatia weledi, uwazi wa taarifa za kifedha, uwajibikaji na kiwango cha juu cha uadilifu wa takwimu.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA Bw. Pius Maneno, alisema Benki ya CRDB imeibuka kinara baada ya kukidhi vigezo vyote vilivyowekwa na taasisi hiyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com