DKT. JAFO APIGA MARUFUKU SHUGHULI ZA UHARIBIFU WA MAZINGIRA CHANZO CHA MAJI MBWINJI - MASASI


***********************************

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo ameonesha kukerwa na vitendo vya uharibifu wa mazingira katika chanzo cha mradi mkubwa wa maji wa Mbwinji unao peleka maji katika wilaya ya Masasi na Nachingwea mkoani Mtwara.

Dkt. Jafo ameonesha hali hiyo wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua shughuli za uhifadhi na utunzaji wa mazingira wilayani Masasi mkoani Mtwara leo Desemba 19, 2021.

Alibaini kuwa chanzo hicho cha maji kinachopokea maji kutoka safu za milima ya Makonde Mna baadhi ya watu wanaofanya shughuli za uchimbaji wa madini, ukataji wa mkaa, pamoja kilimo bila kibali.

“Kitendo chochote kinachohatarisha mazingira ya vyanzo vya maji hakikubaliki na tukifanya mchezo wananchi wa Masasi na Nachingwe watakosa maji na hatutakubali wananchi wetu wapate shida ya kukosa maji kwa sababu tu ya watu fulani, sasa napiga marufuku kuanzia leo shughuli za ukataji mkaa, uchimbaji madini na kilimo,” alisema Jafo.

Kutokana na hali hiyo ya uharibifu wa mazingira, Dkt. Jafo amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kupitia Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira kuanza mchakato rasmi wa kukitanga chanzo hicho kuwa chanzo lindwa kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004.

Aliongeza kuwa mara mchakato huo utakapokamilika eneo hilo litatangazwa kuwa eneo maalumu lililo lindwa na hakutaruhusiwa shughuli zozote za kibinadamu zinazohatarisha mazingira kwa lengo la kuhifadhi chanzo hicho cha maji ambacho ni muhimu kwa wananchi wa wilaya hizo mbili.

Aidha, Waziri huyo wa mazingira ameziagiza kamati za usalama za Wilaya ya Masasi na wilaya zingine zinazo zunguuka safu za milima ya Makonde kusimamia agizo hilo kwa maslahi mapana ya Taifa.

Mradi wa maji wa Masasi - Nachingwea ulibuniwa na kutekelezwa mwaka 2012 na kuigharimu Serikali zaidi ya sh. bilioni 40 kwa lengo la kuwahudumia wakazi zaidi ya laki tatu wa wilaya hizo mbili ambazo zilikuwa na changamoto kubwa ya maji kwa miaka mingi hadi pale serikali ilipoamua kuanzisha mradi huo mkubwa wa maji.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post