GGML YAIDHAMINI GEITA GOLD FC KWA MILIONI 500

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Wayne Louw (kulia) akipeana mkono na Mwenyekiti wa Klabu ya Geita Gold Football Club, Leonard Bugomola (kushoto) baada ya kusaini mkataba wa udhamini wenye thamani ya Shilingi Milioni 500 kati ya GGML na Geita Gold Football Club Desemba 23, 2021 katika halmashauri ya mji wa Geita.


Na Mwandishi wetu - Geita

KAMPUNI ya Geita Gold Mining Limited (GGML imeidhamini Klabu ya soka ya Geita Gold Football Club kwa mkataba mnono wa thamani ya Sh milioni 500 kwa mwaka 2021/2022.

Mkataba huo unaifanya GGML kuwa mdhamini mkuu wa Geita Gold Football Club wenye lengo la kuiwezesha klabu hiyo kushiriki kikamilifu katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa msimu wa Ligi Kuu 2021-2022 na shughuli nyingine za klabu hiyo.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, GGML inapata haki za kuwa mdhamini mkuu wa klabu katika mechi zote au tukio lolote linalohusiana na Msimu wa Ligi Kuu ya NBC kwa mwaka 2021-2022.

Pia GGML inapata fursa ya kuwa mdhamini katika matukio yote yajayo ndani ya klabu kwa kuzingatia sheria na masharti maalum yaliyobainishwa katika makubaliano hayo na kwa mujibu wa Mpango wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii kwa 2021-2022.

Akizungumza wakati wa hafla ya kusaini makubaliano hayo katika Ofisi za Makao Makuu ya Halmashauri ya Mji wa Geita zilizopo Magogo Geita mjini, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Wayne Louw alisema kampuni yake imetia saini mkataba huo kwa sababu inaamini katika kusaidia na kushirikiana kwa manufaa ya pande zote mbili yaani kampuni na jamii inayowazunguka.

“Tumeona watu wa Geita wanapenda soka. Kwa hivyo, kama mshirika na mdau wa Geita, GGML imeamua kuisaidia timu hii ili kutimiza ndoto na malengo ya klabu kwa kuhakikisha inapata mahitaji yote muhimu. Ushindi na kupata kombe ni matokeo ya juhudi za pamoja za wachezaji, uongozi na wadau wote,” alisema.

Aliongeza kuwa fedha hizo za udhamini ambazo Kampuni itatumia kusaidia klabu ni sehemu ya jumla ya bajeti ya Sh bilioni 9.2, ambayo imetengwa kwa ajili ya kutekeleza Mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii wa 2021.

Katika kipindi cha miaka mitatu GGML imetumia zaidi ya Sh bilioni 30 kusaidia maendeleo na ustawi wa jamii inayowazunguka katika nyanja mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Alisema GGML pia imefadhili ujenzi wa Uwanja wa Geita kwa thamani ya shilingi bilioni 1.9 na uwanja huo ukikamilika, utakuwa mkubwa na wa kisasa zaidi wa mjini Geita.

“Miradi hii yote inatekelezwa kwa sababu Kampuni inaona kuwa ni wajibu wa kimaadili kuhakikisha kwamba watu wanaoshiriki katika biashara yetu wanapata maisha bora kwa sisi kuwa hapa,” akasema.

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Wilson Shimo ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo aliipongeza GGML kwa dhamira yake ya kuleta mapinduzi ya soka mkoani Geita.

"Nia ya GGML kufadhili timu yetu inaonyesha jinsi gani kampuni imekuwa karibu na jamii yetu.

“Pia nimeambiwa hapa kwamba GGML imeisaidia Geita Gold Football Club tani 2 za mchele na lita 100 za mafuta ya kupikia kama kifurushi cha Krismasi na mwisho wa mwaka. Nina hakika hilo litawapa motisha ya kushinda mchezo huo muhimu inayoendelea.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Zahara Michuzi alieleza kuwa licha ya kuwa halmashauri ya mji wa Geita na wakazi wa Geita wanamiliki klabu ya Geita Gold Football, GGML waliamua kusaini makubaliano ya udhamini huo kwa sababu pia ni sehemu ya jamii ya Geita.

Zahara Michuzi alifichua kuwa Geita ina vipaji vingi na wanasoka wazuri, sababu zilizoifanya Serikali kuwa na nia ya kuibua uwezo wao kwa kuhamasisha wawekezaji zaidi kuwekeza katika mchezo wa soka.

"GGML ni moja ya mwekezaji mzuri ambaye amekuwa akitekeleza miradi kadhaa endelevu. Uwekezaji wa GGML mkoani Geita umekuwa wa kushangaza,” alisema.

Akitoa maoni yake kuhusu hatua hiyo, Mwenyekiti wa Klabu hiyo ya Geita, Leonard Bugomola aliipongeza GGML kwa udhamini huo huku akiahidi kujitolea na kuhakikisha wachezaji wanakuwa na matarajio ya kufika kileleni mwa ligi kuu.

"GGML imetutia moyo sana. Tuna kitu kimoja tu mbele yetu ambacho ni kucheza na timu kubwa na kuleta kombe mkoani Geita,” alisema.

Tangu kuanzishwa kwake, GGML imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na mamlaka za serikali za mitaa kusaidia miradi kadhaa ya jamii katika mkoa wa Geita kupitia ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi pamoja na programu za kitaifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post