Bila shaka umesikia sana kuhusu hoteli zenye hadhi ya nyota tano katika majiji makubwa duniani kama London nchini Uingereza, Paris nchini Ufaransa, Las Vegas na New York nchini Marekani pamoja na maeneo mengine ya kifahari kama katika visiwa vya Bahamas, Hawaii na kwingineko.
Hata nchini Tanzania, zipo hoteli kadhaa zenye hadhi ya nyota tano, ingawa ubora wake huwezi kufananisha na zilizopo katika majiji yaliyotajwa hapo juu!
Haya ni maeneo ambayo huwezi kumkuta mlalahoi akikatiza, kila kitu kinachopatikana ndani yake kinakuwa na ubora wa hali ya juu, ambao unakwenda sambamba na gharama kubwa kuanzia kwenye vyakula, vinywaji hadi malazi!
Lakini yote tisa, kumi ni Hoteli ya Burj Al Arab iliyopo Dubai, Falme za Kiarabu ambayo ndiyo inatajwa kuwa hoteli bora na ya kifahari kuliko duniani! Yaani mahoteli yote uliyowahi kuyasikia, hayafui dafu kwa Burj Al Arab!
Picha linaanza, unaambiwa hoteli hii ina hadhi ya nyota saba! Tumezoea kusikia hoteli za nyota tano si ndiyo? Sasa hii imevuka huko na kusababisha ipewe hadhi ya Seven Star Hotel na kuwa ya kwanza duniani kote kuwa na hadhi hiyo, na hii ni kwa mujibu wa Mtandao wa Ultra Travel ambao ndiyo ulioitunuku hoteli hii hadhi hiyo.
Unaweza kujiuliza, kwa nini Burj Al Arab imepewa hadhi kubwa kiasi hicho? Kuna nini cha ajabu ambacho hakipatikani katika mahoteli mengine? Twende pamoja hatua kwa hatua, tukiichambua hoteli hii ambayo unaweza kuifananisha na paradiso ndogo ya duniani!
Ufahari wa hoteli ya Burji Al Arab, unaanzia kwenye mazingira ilipojengwa! Imejengwa ndani ya kisiwa maalum kilichotengenezwa na binadamu, Waingereza wanaita Man Made Island, kilichopo mita 280 kutoka Pwani ya Jiji la Dubai maarufu kama Jumeirah Beach!
Ili kuingia ndani ya hoteli hii, ni lazima kwanza upite kwenye daraja maalum lililojengwa baharini, hakuna njia nyingine ya ardhini zaidi ya daraja hilo ambalo nalo lina ulinzi usio wa kawaida, kwa muda wote wa saa 24, siku saba kwa wiki.
Hoteli hii inamilikiwa na Kampuni ya Jumeirah Hotel Group na jengo lake, lina urefu wa mita 210 kutoka usawa wa bahari likiwa na takribani ghorofa 59, na kuifanya ipate sifa nyingine ya kuwa miongoni mwa hoteli zenye maghorofa marefu zaidi duniani!
Tofauti na majengo mengine marefu ya hoteli duniani kama Gevora Hotel, JW Marriott Marquis Dubai, Four Seasons Place Kuala Lumpur na Rose and Rayhaan, Burj Al Arab limejengwa kwa usanifu mkubwa na teknolojia ya kisasa kabisa, likifanana na jahazi kubwa.
Inaelezwa kwamba kisiwa hicho kidogo ambacho hoteli hiyo imejengwa juu yake, kilitengenezwa kwa karibu miaka mitatu mfululizo, ambapo nguzo kubwa na imara zilisimikwa baharini mpaka chini kisha msingi imara ukatandazwa eneo lote ndipo ujenzi wa jengo lenyewe ulipoanza.
Ujenzi wake ulikamilika mwaka 1999 na hoteli ikafunguliwa rasmi Desemba 1, 1999 na kuanza kutoa huduma, jengo lote likiwa limegharibu dola bilioni moja za Kimarekani sawa na shilingi trilioni 2 na bilioni 300 za Kibongo!
Upande wa juu kabisa, kuna uwanja cha helikopta, wenyewe wanaita Helipad ambao wakati mwingine hutumika kwa ajili ya mashindano ya mbio za magari na michezo mbalimbali.
Sehemu kubwa ya jengo hilo, imenakshiwa kwa mapambo ya dhahabu na rangi za kuvutia, kuanzia mwonekano wa nje mpaka mwonekano wa ndani, huku pia ikiwa na fukwe zilizotengenezwa kitaalam pamoja na mabwawa ya kuogelea yaliyojengwa baharini!
Yaani vuta picha, bwawa la kuogelea linajengwa ndani ya bahari na kutenganishwa na maji ya baharini, ndani yake kukiwa na maji safi yasiyo na chumvi hata kidogo! Hiyo ndiyo Burji Al Dubai!
Mandhari ya ndani, kama nilivyoeleza, nayo ni ya kuvutia kuliko maelezo, yaani unaweza kufananisha na Ikulu ya White House ya Marekani au makazi ya Mfalme wa Falme za Kiarabu, mazingira yake yanaonesha wazi kwamba imejengwa kwa ajili ya mabilionea na viongozi wakubwa duniani kwenda kupumzika wakipunga upepo mwanana wa bahari.
Inaelezwa kwamba, idadi ya wahudumu waliopo kwenye hoteli hiyo, inafanya kuwe na uwiano wa wahudumu sita kumhudumia mteja mmoja kwa wakati mmoja, na wahudumu wenyewe siyo watu wa hovyohovyo, ni wale waliopitia mafunzo katika vyuo vikuu na vyuo mbalimbali vinavyotambulika duniani kote!
Unaambiwa pia vyombo vinavyotumika ndani ya hoteli hiyo, kuanzia vijiko, uma, sahani na kadhalika, vimetengenezwa na kunakshiwa kwa dhahabu tupu na tangu ilipofunguliwa miaka takribani 20 iliyopita, kila mwaka imekuwa ikishika nafasi ya kwanza kwa ubora duniani kote, mwaka hadi mwaka!
Ukija kwenye gharama za kulala hotelini hapo kwa usiku mmoja, ndiyo utachoka zaidi! Unaambiwa kwenye vyumba vyenya hadhi ya juu kabisa, Royal Suite, vile vinavyotumika na viongozi wakubwa na mabilionea, inagharimu dola za Kimarekani 24,000 ambazo kwa fedha za Kitanzania, ni takribani shilingi milioni 55!
Rudia tena kusoma kiwango hicho, shilingi milioni 55 kwa usiku mmoja! Ama kwa hakika dunia haina usawa! Wakati wewe ukilia na ugumu wa maisha, wapo watu wanaotumia shilingi milioni 55 kwa malazi ya usiku mmoja.
Basi kwa kifupi hiyo ndiyo Hoteli ya Burj al Arab, hoteli ya kwanza duniani yenye hadhi ya nyota saba!
Social Plugin